Sunday, September 6, 2015

MABANGO YA LOWASSA YAMEZUA BALAA....WANAOYABANDIKA WAWEKWA SELO..DUH

Mabango yenye picha ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, yanayoendelea kubandikwa katika maeneo mbalimbali nchini yamezua kizaazaa, baada ya mengine kuondolewa na wale wanaofanya kazi ya kuyaweka kutishwa na hata kuwekwa ndani na Jeshi la Polisi.
Hali hiyo imejitokeza mkoani Iringa, ambako vijana wanaofanya kazi ya kuweka mabango hayo waliwekwa ndani na Jeshi la Polisi na jijini Dar es Salaam ambako bango lililokuwa limewekwa katika Soko la Kariakoo liliondolewa saa chache tu baada ya kubandikwa na hivyo kuzua mjadala kila kona.
Wakati wale waliokamatwa mkoani Iringa wakidaiwa kuwekwa ndani pasipokuwa na sababu yoyote hadi pale walipotolewa na maofisa wa Chadema, Jijini Dar es Salaam bango hilo liliondolewa na uongozi wa Soko la Kariakoo kwa madai ya kubandikwa kimakosa.
Juzi saa 12 jioni wafanyakazi wa kampuni ya Platnum Media Co. Ltd walifika sokoni hapo na kuanza kubandika bango hilo lililokuwa na picha ya Lowassa, ikiambatana na maandishi yanayosomeka; ‘Edward Lowassa…Ni wakati wa mabadiliko’.
Wakati bango hilo likibandikwa umati mkubwa ulikusanyika karibu na eneo hilo na kuanza kushangilia, huku wengine wakiimba “Rais…rais…rais”.
Meneja wa Soko la Kariakoo, Florens Seiya, alisema yeye ndiye aliyetoa amri ya kuondolewa kwa bango hilo kwa kuwa soko hilo ni taasisi ya umma na hairuhusiwi kuwekwa mabango ya kampeni.
Ni kweli tunamfahamu aliyebandika bango hilo, ni mtu ambaye tuna mkataba naye wa kutumia ubao huo kubandika mabango, lakini hili lilibandikwa kimakosa bila kutushirikisha,” alisema Seiya.
Alisema katika mkataba wa soko hilo na kampuni ya Platnum Media Co. Ltd, kifungu cha sita kinamtaka aonyeshe maudhui yaliyomo katika mabango kabla ya kubandika, kitu ambacho yeye (Platnum) hakufanya.
“Jana (juzi) baada ya kufunga ofisi na kuondoka ndipo alipofika na kuanza kuweka bango hilo, jambo lililofanya watu wakusanyike kwa wingi utafikiri pana mkutano wa siasa huku wengine wakishangilia,” alisema Seiya.
Alisema kutokana na soko hilo kuwa ni taasisi ya umma, hairuhusiwi kuweka tangazo lolote linalohusu kampeni za kisiasa kwa kuwa wao hawafungamani na chama chochote.
Mtanzania imeonyeshwa barua hiyo yenye kumbukumbu namba SKM/B/125 iliyokuwa na kichwa cha habari ‘ukiukaji wa mkataba wa matangazo’ ya Septemba 4 mwaka huu, iliyomtaka Platnum ajieleze.
Chanzo:gazeti la Mtanzania