Wanafunzi wa shule mbili za msingi za Kiriba “A” na kiriba “B” katika halmashauri ya Musoma vijijini mkoani Mara wanalazimika kusomea chini ya miti baada ya shule hizo katika kijiji cha kiriba kukabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa hatua ambayo pia imekuwa ikisababisha kupewa likizo za mara kwa mara hasa wakati wa msimu wa mvua na hivyo kulazimika kukosa masomo.
Wakizungumza wakati wa Harambee ya kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya Madarasa,Vyoo na Nyumba za walimu katika shule hizo,baadhi ya walimu wakiwemo walimu wakuu wa shule hizo,wamesema upungufu huo mkubwa wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ya shule imekuwa ikisababisha wanafunzi kusoma katika mazingira magumu hasa wakati wa mvua na jua kali.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kiriba Bw.Semeni Mkama,akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho,amesema uongozi wa kijiji utalazimika sasa kutunga sheria ndogondogo kwa ajili kusaidia ukusanyaji wa michango kutoka kwa wananchi ili kuwezesha upatikanaji wa haraka wa fedha za ukarabati na ujenzi wa miundominu hiyo ya elimu katika shule hizo na hivyo kuwandolea adha mhiyo kubwa wanayoipata wanafunzi na walimu wao.
Kiasi cha zaidi shilingi milioni 44.8 kinahitajika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi huo wa miondombinu katika shule hizo huku harambea hiyo ikifanikiwa kukusanya fedha taslimu na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 8.7.