Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameendelea kujinadi katika kampeni zake, huku akitumia kauli mbiu ya Movement for Change (M4C) inayotumiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye mikutano yake.
Chadema hivi karibuni waliilalamikia hatua hiyo ya Dk. Magufuli na kumtaka aache kutumia kauli mbiu hiyo ambayo ina maana ya ‘vuguvugu la mabadiliko’, huku wakitishia kumpandisha kizimbani kwa kile walichoeleza ni alama yao waliyoisajili.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa mpira wa Kyerwa Mjini, mkoani Kagera juzi, mgombea huyo wa CCM aliuambia uliojitokeza kumsikiliza kuwa kama wanataka mabadiliko wamchague yeye kwasababu yeye ndiye mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli na kuibadilisha kauli mbiu hiyo kwa kuweka jina lake: Magufuli for Change (M4C).
“Mimi ni Magufuli for Change, haya imbeni Magufuli for Change,”aliwaambia wananchi hao ambao nao walianza kuimba wakimfuatisha.
Katika mkutano huo, Dk. Magufuli pia alimrushia kijembe Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, ambaye amekuwa akizunguka na mgombea urais aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa na kuinanga serikali kuwa haijafanya lolote kwa miaka yote tangu uhuru.
Ingawa hakumtaja kwa jina, Dk. Magufuli alisema kuna mtu alikuwa na madaraka makubwa serikalini ambaye alidumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10 lakini amekuwa akiilalamikia serikali aliyokuwa akiitumikia.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa kwa kipindi cha miaka 10 mfulizo.
“Mtu alikuwa msaidizi wa karibu wa Rais na amekaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10 mfululizo anasema hatujafanya kitu, ina maana yeye ndiye aliyetukwamisha akiwa madarakani,” alisema.