Saturday, September 26, 2015

Mgombea CCM akitabiria anguko chama chake

Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki kwa tiketi ya CCM.

MGOMBEA ubunge Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki (CCM), amesema chama hicho kilikuwa hakina uwezo na nguvu ya ushindi katika jimbo hilo, kabla ya kumteua Dk. John Magufuli, kuwania nafasi ya urais, kwa kuwa wananchi walikuwa wamekichoka.Anaandika Moses Mseti, Tarime … (endelea).
"Amesema kitendo cha mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, chini ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kujiunga na upinzani kimesababisha mtikisiko na mpasuko ndani ya CCM wilayani humo.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Kembaki amesema baada ya CCM kumteua Dk. Magufuli kugombea urais, amesaidia kurudisha matumaini kwa wanachama, wagombea ubunge na udiwani   ambapo hivi sasa wamethubutu kuonekana mitaani wakiwa wamevaa mavazi ya chama hicho tofauti na ilivyokuwa awali.
Kembaki amesema ujio wa Dk. Magufuli umewapa nguvu wagombea wa CCM pamoja na wananchama wake katika kukitetea chama kwa kueleza mazuri yaliyofanywa na mgombea huyo kwa miaka 20 akiwa waziri wa wizara mbalimbali.
Amesema kutokana na hali hiyo, ushindani uliopo kati yake na mgombea wa Chadema, Esther Matiko, umekuwa mkali na hakuna aliye na uhakika kuibuka mshindi kwa sababu wakazi wa Tarime huwa hawatabiriki hadi siku ya mwisho wa kampeni.
“Ni jambo ambalo huwezi kulificha kwa wakazi wa Tarime walivyokuwa wakikichukia chama chetu tena hadharani, yaani hata kutembea na kofia au fulana ilikuwa shida kwa sababu utapigwa, kitendo hiki cha wananchi kukikataa chama chetu hadharani kilitupatia shida sana lakini Mungu hamtupi mja wake kwani ujio wa Dk. Magufuli umerudisha matumaini kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Lakini hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Lowasa kuhama CCM na kujiunga Chadema, hakika upepo ulibadilika lakini kutokana na utendaji wa Dk. Magufuli alionao umesaidia sisi wagombea kukitetea chama na kueleza mazuri na mabaya ya mgombea wa upinzani, hivi sasa wananchi wameanza kuelewa na kutuunga mkono,” amesema.
Kembaki alidai kuwa tangu awali fikra za wananchi zilikuwa ni kuiondoa CCM madarakani, lakini kadri walivyoendelea kuwaelimisha kwa kutaja mambo yaliyofanywa na Dk. Magufuli, wananchi waliweza kubadilika na sasa wanakimbizana na UKAWA.
“Wananchi wa Tarime hawataki udanganyifu, ukiwadanganya ujue unatafutwa kupigwa, ndio maana sisi wagombea tunasema vitu ambavyo tuna uwezo navyo na kama tutavisema tukashindwa kuvifanya inakula kwetu,” amesema.
Kembaki ambaye wazo la kugombea ubunge Jimbo la Tarime Mjini alikuwa nalo miaka 10 iliyopita ambapo alianza kuonyesha uwezo wa kuwasaidia wananchi na kuwaletea maendeleo kwa kujitolea kujenga barabara kutoka Uhemba hadi Tagota yenye kilomita 10, kuviwezesha vikundi vya walemavu, wajane, vijana, akina mama na wazee.
Pia amesema alijenga zahanati katika Kata mbalimbali zikiwamo Kenyamanyori, Magena na Kimusi pamoja na shule za msingi za Mtahuru, Nyamwino na Gimenya.
Kembali amesema mbali ya miradi hiyo alianzisha mashindano ya mchezo wa mpira maarufu Kembaki Cup kitendo kilichosababisha vijana wengi kupata ajira baada ya kuchukuliwa na timu kubwa.
Hata hivyo amesema umefika wakati wagombea kuacha kusema kwenye mikutano kwamba watawafanyia kitu gani wananchi bali wanapaswa wakaeza walichokifanya ili wananchi wenyewe waone kwa macho yao.