AIBU! Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zuhura maarufu kama Lolo Princessa ambaye ni mpenzi wa kijana anayejulikana kama Koko Byanco juzikati alijikuta akipata aibu kubwa baada ya kufumaniwa akiwa na mwanaume mwingine kiasi cha kusababisha mchepuko huo kujitosa baharini katika ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam kukwepa kipigo.
Mapema, dawati la Oparesheni Fichua Maovu (OFM) lilipata taarifa kutoka kwa Koko, akilalamika kuwa amenasa meseji kwenye simu ya mtu wake, ikionyesha mawasiliano na mwanaume mwingine, wakipeana ahadi ya kukutana ufukweni siku hiyo, ambazo zilikuwa na viashiria vyote vya kimahaba.
“Mpaka nimeamua kuja kwenu nataka mnisaidie jamani maisha yangu hayana amani kabisa, naomba mnisaidie nimnase mbaya wangu na hii tabia ikome kwa wote wenye mambo kama hayo. Mbaya zaidi kwao hawajui kama ananisumbua, hivi nataka mashemeji zangu wamuone ndugu yao anachonifanyia,” alisema Koko.
Baada ya kuwaona huku makamanda wa OFM wakianza kukusanya ushahidi kwa kupiga picha, mwanaume alishindwa kuvumilia na kuanzisha timbwili kali kwa mgoni wake, ambaye alipoona ‘jeshi’ kubwa likimsogelea, alilazimika kukimbilia ndani ya bahari huku akifukuzwa na mwenye mali.