Friday, October 16, 2015

Magufuli Akiri Mafisadi Yako Ndani ya CCM.......Ameahidi Akiingia Ikulu Atawashughulikia Bila Woga. Pia kasema Mawaziri Wote Atawasainisha Mikataba


Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema mafisadi wamo hadi ndani ya chama chake na ndiyo maana baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wengi wao wameanza kuweweseka kutokana na hofu kubwa waliyo nayo dhidi yake.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni ya chama chake mjini Kisarawe, Pwani na baadaye Ukonga, jijini Dar es Salaam jana, Magufuli alikiri kuwa chama chake kiliwalea walarushwa na mafisadi kwa muda mrefu na ndiyo maana baadhi ya watu walianza kukichukia.

Hata hivyo, alisema tatizo hilo halitakuwapo tena kwani atakapoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, atahakikisha kuwa mafisadi wote wanashughulikiwa bila woga.

“Ndugu zangu, nasema kweli mafisadi hawako upinzani tu... ni ngumu sana mtu aliye ndani ya CCM kuyasema haya, lakini lazima niseme ukweli maana msemaukweli ni mpenzi wa Mungu. Haya mafisadi ndiyo yametufikisha hapa na (sasa), lazima tuyashughulikie,” alisema Magufuli na kushangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wake wa Ukonga.

Magufuli aliwataja kwa sifa za jumla mafisadi waliopo kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali, ambao hujihusisha na vitendo vya rushwa na dhuluma dhidi ya wananchi kiasi cha kuifanya serikali ichukiwe na baadhi ya wananchi wake.

Akitolea mfano, Magufuli alisema ni aibu kuona serikali ikikimbizana na mamalishe na wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) ili kupata kodi wakati kuna baadhi ya nchi ambazo zinaendeshwa kwa mapato ya bandari tu.

Magufuli aliongeza kuwa anatambua wananchi wamekuwa wakinyanyaswa katika maeneo mbalimbali ikiwamo kutozwa kodi zisizosaidia kuinua pato la taifa bali kuwafaidisha baadhi ya viongozi na kwamba, kwa sababu hiyo, haoni sababu ya kuendelea kwa hali hiyo hasa kwa kujua kuwa kuna nchi zinajiendesha kwa mapato ya bandari.

Alisema yote hayo ni baadhi ya mambo anayoamini kuwa ni sababu ya yeye kuchaguliwa kuwa rais ili kudhibiti uonevu kwa wanyonge na pia kupambana na mafisadi serikalini, ambao wamezoea kuishi kwa rushwa na ulaghai.

Kwa mfano, alisema anajua namna ambavyo baadhi ya watumishi bandarini huruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na kuikosesha serikali mapato yake ili kuwahudumia wananchi.

“Wapo watu wanaikosesha serikali mapato. Hawa nataka nikapambane nao... na nitapambana nao kweli kweli. Na hawatanikwepa…najua wananiogopa na wameanza kumwaga hela ili nishindwe. Nyinyi hela zao kuleni maana ni kodi zenu, lakini kura ni kwa Magufuli,” alisema.

Barabara  za  juu  Tazara
Katika hatua nyingine, mgombea huyo alisema ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya Tazara, Dar es Salaam utaanza muda wowote kwani mkandarasi ameshapatikana.

Dk. Magufuli alisema kuwa serikali ya Tanzania imeshatiliana saini na serikali ya Japan kwa ajili ya ujenzi huo kwani hata michoro imeshakamilika.

Alisema katika makutano ya Ubungo, kutajengwa barabara ya juu ya ghorofa tatu ili kuwezesha magari mengine kupita juu, mengine katikati na mengine chini ili kupunguza msongamano.

Aahidi Kuwasainisha Mikataba Mawaziri Wake
Kuhusiana na uteuzi wa baraza lake la mawaziri, Magufuli alisema atateua mawaziri wachapakazi na si wale wa kukaa ofisini huku shughuli nyingi za maendeleo zikikwama.

Alisema anataka mawaziri atakaowateua kuiga mfano wake kwa kushinda kwenye miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Dk. Magufuli alisema kama yeye angekuwa mtu wa kushinda ofisini na kutoa maagizo, huenda barabara za lami zinazofikia kilomita 17,000 zisingekuwapo kwani makandarasi wengi walionyesha uzembe aliwafukuza.

“Kama mimi nilianguka kwenye helikopta (chopa) nikikagua mafuriko Dar es Salaam, nikalala daraja la Dumila Morogoro, nao wafanye hivyo…kama ni Waziri wa Maji, basi ashinde kwenye miradi ya maji, kama ni barabara basi ashinde barabarani kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango,” alisema na kuongeza.

“Nikishinda na kuingia Ikulu nitakuwa nawahoji mawaziri nitakaowateua kama watamudu majukumu yao ama la na yule atakayekubali kwamba anaweza basi atasaini na akishaini ole wake nimpe kazi halafu ashindwe kumudu majukumu  yake.”

Awapiga kijembe wanaofagia barabara
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwashangaa wanaopiga deki barabara za lami ili wagombea wao wapite huku wakibeza kwamba serikali ya CCM haijafanya lolote.

Aliwataka waendeleze utaratibu wa kupiga deki barabara ili ziwe safi hata baada ya uchaguzi ili kuwaonyesha ni namna gani serikali ya CCM imejenga barabara nyingi za lami.

“Huwezi kupiga deki barabara ya vumbi, huwezi kupiga deki barabara yenye mashimo, wanatusema wakati wanapita kwenye barabara hizo hizo za lami tulizojenga,” alisema Magufuli.

Hivi karibuni, baadhi ya wananchi wa mji wa Musoma mkoani Mara   na  Mkoani Mwanza walijitokeza kupiga deki barabara kabla ya kutumiwa na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa. Mbali na Chadema, Ukawa inaundwa na CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.