Hata hivyo, uongozi wa Azam umebainisha kuwa upotevu wa makontena hayo hauhusishi bidhaa zinazomilikiwa na kampuni hiyo na kwamba umejitoa kwa hali na mali kufanikisha uchunguzi wa sakata hilo.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Kamishna wa Forodha wa TRA, Wolfgang Salia kwa Meneja Mkuu wa Said Salim Bakhresa & Co Ltd, kampuni hiyo imezuiwa kupeka mizigo kwenye Bandari kavu namba 003.

“Kutokana na suala hilo, imeamriwa kuwa upelekaji wa mizigo katika bandari yako ya nchi kavu usimamishwe mara moja kuanzia siku ya tarehe ya barua hii hadi hapo itakapoamuliwa. Wadau wote wanaohusika wanatakiwa kufuata amri hii,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, 2015.
Barua hiyo iliyoandikwa siku 10 kabla ya ziara ya Waziri Mkuu, na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, ilisema uondoshaji wa mizigo katika eneo hilo kwenda kwa wateja utaendelea kama kawaida.

