Sunday, December 20, 2015

Mwakyembe: Tutamalizia Mchakato wa Katiba Mpya Kuanzia Pale Ulipoishia


Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais amempa kazi ya kuhakikisha anakamilisha mchakato wa Katiba Mpya pamoja na uanzishwaji wa Mahakama ya Rushwa.

Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ilipangwa kufanyika Aprili 30, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikatangaza kuiahirisha hadi itakapotangazwa tema, ikisema inataka kukamilisha kwanza uandikishaji wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.

Lakini kabla ya kutangaza kuahirisha kazi hiyo, vyama vya upinzani, ambavyo vilisusia Bunge la Katiba kwa madai kuwa lilikiuka utashi wa wananchi kwa kuweka kando sehemu kubwa ya mapendekezo yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba, walikuwa wakitaka mchakato huo uanze upya.

Lakini jana, Dk Mwakyembe alisema moja ya majukumu aliyopewa ni kuhakikisha anakamilisha mchakato huo wa kuunda Katiba Mpya ulioanza miaka mitatu iliyopita wakati Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipotangaza kuanza rasmi kuwa Serikali itaanza kazi ya kuandika Katiba Mpya.

“Kuna masuala mengi ambayo wizara yangu inahusika nayo, mengine bado sijayaelewa vyema kwamba yapo kwenye hatua gani, lakini suala la Katiba Mpya hilo ni jukumu ambalo hata Rais alinitamkia kuwa amenikabidhi niliendeleze kwa hatua iliyobaki,” alisema Dk Mwakyembe.

Kauli yake Dk Mwakyembe ambaye amebobea kwenye sheria, haikupokelewa vizuri na wanasiasa wa upinzani ambao walisema kutekelezwa kwa mpango huo kutakuwa ni kuanzisha tena mgogoro bila ya sababu za maana, na kwamba upatikanaji wa kura za Wazanzibari walioko Bara bado haujapatiwa ufumbuzi.

Akizungumzia tamko hilo la Dk Mwakyembe, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ikiwa Serikali inataka kuendeleza mchakato wa Katiba, ikubali kuunda upya Bunge la Katiba kwa mujibu wa sheria.

“Sheria ya Kura ya Maoni haina utaratibu wa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya na hairuhusu kupata tarehe mpya ya kupiga kura ya maoni baada ya kuahirisha upigaji kura,” alisema mwanasheria huyo wa kujitegemea.

“Kama Mwakyembe ataendeleza upya mchakato huu, aanzie alipoishia Jaji (Joseph) Warioba.”

Bunge la Katiba liliingia dosari baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine kutoka taasisi tofauti, kususia vikao wakidai kuwa mapendekezo ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba, ambayo iliongozwa na Jaji Joseph Warioba, yalitupwa na badala yake yakawekwa mapendekezo ya CCM.

Wajumbe hao walitoka wakati Bunge la Katiba likiwa limekwama kwenye Sura ya Kwanza na ya Sita zinazozungumzia Muundo wa Muungano, baada ya Tume ya Warioba kuwasilisha mapendekezo yanayotaka serikali tatu, huku wajumbe wengi wa chombo waliotoka CCM wakitaka uendelee muundo wa sasa wa serikali mbili.

Pamoja na wajumbe wa vyama hivyo vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujiengua, Bunge la Katiba liliendelea na mchakato na kufikia kupitisha Katiba inayopendekezwa ambayo ingepigiwa kura na wananchi Aprili 30, lakini haikuwezekana.