Baada ya kuibua ufisadi wa makontena 2,431 na mengine 349 kupitishwa bila ushuru, Rais Magufuli alitoa muda wa siku saba kwa wahusika kujitokeza kulipia kodi, baadhi waliitikia wito lakini inaonekana bado wanajaribu kujificha.
Jana, ilibainika kuwa makontena 11,884 na magari 2,019 yenye thamani ya Sh48 bilioni yamepitishwa kwenye bandari kavu bila kulipiwa tozo za bandari.
Ufisadi huo umeibuka baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya ukaguzi mwingine katika bandari kavu (ICD) na maghala ya ushuru wa forodha (CFS) na kubaini upotevu wa kiasi hicho cha fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu makontena na magari yaliyotolewa katika bandari kavu na maghala ya ushuru wa forodha ni kuwakamata watumishi 15 wa Bandari waliohusika katika ukusanyaji wa tozo hizo na tayari wameshafikishwa polisi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Hii inatokana na ukaguzi wa awali uliofanyika katika bandari kavu nne ambazo zilionyesha upotevu wa mapato na ndipo, TPA iliamua kufanya ukaguzi mwingine katika ICD na CFS zote na hivyo kubaini upotevu wa Sh48 bilioni za mapato ya Bandari,” alisema Profesa Mbarawa.
Makontena hayo pamoja na magari yalitolewa ICD na CFS baada ya TPA kufanya ukaguzi katika bandari hizo na kubaini upotevu huo wa mapato.
“Makontena 11, 884 yenye thamani ya Sh47,418,474,795 yalitolewa ICD na CFS bila kulipia tozo ya bandari na hivyo kuisababishia bandari upotevu wa kiasi hicho cha mapato,” alisema. “Pia, magari 2,019 yenye thamani ya Sh1,072,485,518 yametolewa ICD na CFS bila kulipiwa tozo za bandari na tayari hatua kali tumeshachukua kwa kuwakamata watumishi saba kati ya 15 wa Bandari.”
Profesa Mbarawa alisema magari yaliyotolewa kutoka kwenye maghala sita ya ushuru wa forodha bila kulipia tozo ya bandari ni TALL iliyotoa magari 309 yenye thamani ya Sh242,481,207, Chikasa (magari 65, ya Sh16,370,360) na Farion (magari 18 ya Sh46,390,385).
Magari mengine ni kutoka ghala la Silver iliyotoa magari 97 yenye thamani ya Sh168,904,390, Mass (magari 171, ya Sh32,807,115) na Hesu (magari 1,359 ya Sh565,533,061) bila malipo ya tozo za bandari ambazo ni jumla ya Sh1.07.
Hatua zilizochukuliwa
“Kutokana na upotevu huo, watumishi 15 wa TPA waliokuwa wanahusika na ukusanyaji wa mapato hayo, wamekamatwa Desemba 28 (juzi) na kufikishwa polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Profesa Mbarawa.
Aliwataja watumishi hao wa Bandari kuwa ni Nathan Edward, John Elisante, Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Happygod Naftal, Adnan Ally, Masoud Seleman, Bonasweet Kimaina, Bernadeta Sangawe na Zainabu Bwijo.
“Serikali haitamvumilia mfanyakazi yeyote wa TPA awe mkubwa au mdogo ambaye ataendelea kujihusisha na upotevu wa mapato ya Bandari,” alisema.
Alisema Serikali itawafutia leseni za biashara mawakala wote wa forodha ambao wataendelea kushirikiana na wafanyakazi wa Bandari kutoa mizigo bila kulipia tozo hiyo.
Mawakala na vielelezo
Wakati huohuo, waziri huyo amewataka mawakala 280 wa forodha ambao wanatuhumiwa kuhusika na kutolewa kwa makontena na magari bila malipo ya tozo, kupeleka vielelezo vya uthibitisho ndani ya siku saba kuanzia jana.
“Watakaoshindwa baada ya muda huo tulioweka watakamatwa na kufikishwa polisi ili walipe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa kufanya biashara na Bandari,” aliongeza.
Katika tangazo lake kwenye vyombo vya habari jana, TPA ilitangaza kampuni 243, nyingi zikiwa za forodha za uchukuzi zikiwamo Ballore Africa Logistics, Cargo Stars Limited, Mohamed Enterprises Tanzania Limited, Quality Logistics (T) Limited, Said Salim Bakhresa na Sbc Tanzania Limited, ikizitaka kupeleka nyaraka zao za kuanzia Julai 2014 hadi Aprili kwenye ofisi za meneja biashara na masoko kwa ajili ya kuhakiki malipo waliyofanya TRA.
Naibu mkurugenzi makampuni ya Said Salim Bakhresa, Hussein Sufiani Ally alisema makontena yote ya kampuni hiyo yaliyotolewa bandarini yalilipiwa.
“TPA wametoa hilo tangazo kwa sababu wanafahamu tumelipa ila wanataka tupeleke nyaraka zetu kwa sababu wanataka kujiridhisha,” alisema Ally.
Alipoulizwa kuhusu taarifa ya Profesa Mbarawa aliyotaja Azam ambayo inamilikiwa na Said Salim Bakhresa kuwa ina makontena 295 ambayo yalitolewa kwenye bandari kavu bila kulipiwa tozo, alisema hajapata taarifa hizo.
Sh900 milioni zalipwa
Katika hatua nyingine, jumla ya Sh900 milioni zimelipwa kuanzia Desemba 7 hadi 28, baada ya mawakala wa forodha kulipa tozo ya Bandari kwa makontena 2,431 yaliyokamatwa na Waziri Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza TPA.
Waziri Mbarawa alisema kati ya mawakala 55 wa forodha ambao walitakiwa kulipa kwa hiari ndani ya siku saba, ni saba tu waliolipa kwa wakati kiasi cha Sh80 milioni.
“Baada ya muda ulitolewa na Serikali kuisha, mawakala ambao walikuwa hawajalipa walisitishiwa kufanya biashara na TPA hadi watakapolipa na tayari hadi juzi askari wamefanikiwa kuwakamata watu 15 kati yao ambao walilipa Sh820 milioni walizokuwa wanadaiwa na kufanya kiasi kilicholipwa mpaka sasa kuwa Sh900 milioni,” aliongeza.
Alisema kazi ya kuwakamata mawakala ambao bado hawajalipa inaendelea na lengo la Serikali ni hadi kufikia Januari 10, mwakani mawakala wote wa forodha wawe wamekamatwa na kufikishwa polisi ili walipe kwa nguvu. CHANZO : MWANANCHI