Sunday, January 24, 2016

HIVI NDIVYO MWALIMU MKUU ALIVYOFUMWA AKICHANGISHA MICHANGO SHULE NA JEMEDARI WA RAIS MAGUFULI





WAZIRI  wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene amefanya ziara ya kushutukiza katika shule ya msingi Dodoma Makulu katika manispaa ya Dodoma baada ya kubaini mkuu wa shule ameitisha wazazi kwa kutaka wachangie.

Suala hilo limekuwa kizungumkuti kufuatia Ofisa Elimu shule ya Msingi wa manispaa ya Dodoma, Scola Kapinga kuandika barua kwa shule za msingi katika manispaa yake mkoani hapa kuzitaka kuchangisha michango mbalimbali.

Hali hiyo kumepelekea Simbachawene akiambatana na Naibu katibu mkuu Tamisemi Elimu, Bernard Makali kufanya ziara ya kushtukiza katika shule hiyo ilo  kujionea hali halisi ya mgawanyo wa fedha za elimu bure huku wazazi wakichangishwa .

Waziri huyo akizungumza na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Janeth Justine alimuhoji kuhusiana na uendeshaji wa elimu katika shule hiyo pamoja na kutaka kujua idadi ya wanafunzi.

Mwalimu huyo alijibu kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,400 na ilipokea fedha za elimu bure jumla ya Sh. 152,000 milioni na walizigawanya fedha hizo kulingana na waraka namba 6 wa serikali.

“Asilimia 30 vifaa, asilimia 30 ukarabati, mitihani asilimia 20 ambapo kwenye michezo ni asilimia 10 huku utawala ni asilimia 10 lakini pia nilipokea barua toka Manispaa ikielekeza kuwachangisha wazazi fedha za mlinzi, umeme na maji.

“Nilivyopokea barua niliitisha kikao jana cha wazazi (juzi) ambapo wazungumzaji alikuwa diwani wa Kata hiyo, Paschal Matula aliwataka wazazi kukubaliana kutoa michango hiyo mlinzi Sh. 50,000, Maji Sh. 72,000 na umeme kiasi cha Sh 150,000 kwa mwaka,” amesema Mwalimu Janeth.

Hata hivyo amesema kuwa katika kikao hicho hawakufikia muafaka baada ya wazazi kuweka mgomo juu ya kuchangia michango hiyo.

Kufuatia kuwepo kwa michango hiyo Waziri huyo alitoa agizo kwa Wakurugenzi, wakuu wa Wilaya na wakuu wa mikoa nchini kusoma vizuri waraka namba 6 uliotolewa na Serikali kuhusu mchanganuo wa elimu bure na kuacha kuchangisha michango wazazi isiyokuwa ya lazima.

“Inaonekana kuna watu wanataka kujinufaisha na michango hiyo kupitia wazazi kwani michango ambayo wazazi walikuwa wanatakiwa kuchanga tayari serikali ilishalipa michango yote na walimu wakuu walishakabidhiwa,” amesema Simbachawene.