Monday, January 11, 2016

January Makamba Atembelea Na Kujionea Athari Za BomoaBomoa Dar........Aagiza Serikali Za Mitaa Kufanya Tathmini Ili Kubaini Familia Zinazohitaji Msaada wa Kibinadamu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, jana alitembelea maeneo ya  mabondeni  yaliyokumbwa na Bomoabomoa ili kujionea hali halisi ya wananchi ilivyo.

Akizungumza mara baada ya ziara yake , January alisema  kila utaratibu lazima ukumbwe na changamoto, hivyo ,safari hii, kabla ya nyumba kubomolewa, lazima kila moja ifanyiwe tathmini kwanza.

“Kila utaratibu lazima ukumbwe na changamoto na sisi tumezibainisha na kuzifanyia kazi, ni kweli wapo waliobomolewa lakini walipewa hati na vibali vya ujenzi vya Serikali, ukweli ni kwamba kati ya makazi 774 yaliyokwishabomolewa ni makazi 20 tu ndiye yenye hati hizo,” alisema January.

Pia,alisema serikali imeagiza Ofisi za Serikali za Mitaa katika maeneo yaliyobomolewa, kufanya tathmini na kuangalia familia zinazohitaji msaada wa kibinadamu zisaidiwe. 

Hata hivyo, alisema Serikali imebaini kuwa wananchi wengi ambao nyumba zao zimebomolewa, takribani asilimia 70 ni wapangaji na wenye nyumba wapo ambao walishafidiwa maeneo hayo na kuondoka, lakini baadaye wakarejea.

Alisema katika ziara yake hiyo ya jana, kuna maeneo ya aina tatu ambayo ni yaliyokwishabomolewa, yaliyowekwa alama ya X lakini hayajabomolewa na yaliyo katika mazingira hatarishi, lakini hayajawekewa alama. 

Alisema katika eneo la waliowekewa alama kabla ya kubomolewa, aligundua wananchi wengi wako katika taharuki, ingawa walikiri na kuonesha kufahamu kuwa mazingira wanayoishi ni hatarishi.

“Nilizungumza nao na wametaka watafutiwe maeneo mbadala lakini pia tumeona kuwa kwa sababu wengi wao ni wapangaji, Serikali haina uwezo wa kuwatafutia maeneo mbadala, hivyo tumewaambia wale wapangaji ni vyema wakapange maeneo mengine salama,” alisisitiza. 

Alisema watakaowekewa utaratibu mbadala ni watakaobainika kuwa nyumba zao, zina hati zilizotolewa na Serikali, lakini pia kupatiwa vibali vya ujenzi.

Aidha, Waziri alisema katika maeneo mengine alikotembelea, alikuta ni familia chache zilizokwishabomolewa. 

Wenye hali tete
 Alisema katika eneo la Mkwajuni, kulikuwa na familia nne zinazoishi katika vifusi vya nyumba zao zilizobomolewa.

“Ndio maana nikaagiza ofisi za Serikali za Mitaa kuangalia na kutambua familia zinazohitaji msaada wa kibinadamu zilizokumbwa na utaratibu huu wa bomoabomoa,” alisema.

Alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha nyumba hizo zinabomolewa kwa kufuata mazingira ya kibinadamu, lakini pia alisisitiza ni lazima sheria zifuatwe kwa kuhakikisha wanaoishi kwenye maeneo hatarishi, wanaondolewa kabla ya kukumbwa na hatari.

Alisema Serikali inatekeleza ubomoaji wa nyumba hizo kwa nia ya dhati ya kuwahakikishia wananchi hao usalama, kwani katika maeneo hayo mvua kubwa zikinyesha, maisha yatakuwa hatarini.

January alisema katika mvua zilizonyesha mwaka 2011, takribani wakazi wa mabondeni 49 walipoteza maisha, na mwaka huu tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ilishatangaza uwezekano wa kutokea mvua za El-nino. Alisema ni muhimu wananchi wakahama haraka maeneo hayo.

Jambo lingine alilosema ameshuhudia kupitia ziara hiyo ya jana, ni baadhi ya nyumba zilizo hatarini ambazo pamoja na kutokuwepo kwa mvua, lakini nyumba hizo ziko kwenye maeneo oevu na kuzungukwa na maji.

 Nyumba nyingine zimebainika zikitiririsha maji machafu ya chooni kwenye mito na mabonde yanayotumika katika shughuli za kilimo cha mboga.