Sunday, February 7, 2016

AZAM FC YAREJEA NA MOTO LIGI KUU, YAITANDIKA 1-0 MWADUI...TOTO YAIPIGA 2-1 COASTAL

Kagera Sugar 0-1 Simba SC
Mbeya City 0-0 Prisons
JKT Ruvu 0-4 Yanga SC
Ndanda FC 1-1 Mtibwa Sugar
Azam FC 1-0 Mwadui FC
Toto Africans 2-1 Coastal Union
Majimaji 1-0 Mgambo JKT
Februari 6, 2016
African Sports 0-0 Stand United

Kipre Tchetche ameing'arisha Azam FC leo

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
BAO pekee la mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche limaipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kipre Tchetche, mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Ivory Coast, alifunga bao hilo dakika ya 18 akimalizia pasi ya Nahodha John Bocco.
Na kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 42 baada ya kucheza mechi 16, ikizidiwa pointi moja na mabingwa watetezi, Yanga SC waliocheza mechi mbili zaidi.
Azam FC sasa inafungana kwa pointi na Simba SC, inayokaa nafasi ya pili kwa wastani wake mzuri wa mabao, ingawa na wao wamecheza mechi mbili zaidi. 
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Simba SC imeshinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Yanga SC imeshinda 4-0 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Mbeya City imetoka sare ya 0-0 na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya. 
Ndanda FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Toto Africans imeshinda 2-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Majimaji imeshinda 1-0 dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Majimaji, Songea, wakati jana African Sports ilitoa sare ya 0-0 na Stand United Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Serge Wawa, Jean Mugiraneza, Himid Mao/Kipre Balou dk70, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Frank Domayo dk78, Ramadhani Singano ‘Messi’, Kipre Tchetche/Allan Wanga dk66na John Bocco.