Saturday, March 12, 2016

Kipa Simba augua kansa

 
 
MAISHA ya kisoka ya kipa wa zamani wa Simba, Abel Dhaira ni kama yamefikia tamati baada ya Mganda huyo kukumbwa na masaibu mazito. Dhaira, kipa mrefu aliitumikia Simba msimu wa 2012/2013 amegundulika kupata tatizo la saratani (kansa) ya utumbo baada ya kufanyiwa uchunguzi na jopo la madaktari nchini Iceland ambako alikuwa akicheza soka la kulipwa kwenye timu ya IBV Vestmannaeyjar.
Klabu hiyo ya Iceland imetoa taarifa juu ya tatizo hilo lililomsibu Dhaira aliyewahi kuidakia pia timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ akisaidiana na Denis Onyango.
“Abel amekuwa mgonjwa sana miezi ya karibuni. Yupo Uganda mwaka sasa akisumbuliwa na kansa ya utumbo ambayo sasa inasambaa kwa kasi kwenye viungo vingine.
Makampuni yanayotudhamini yamekubali kusimama nasi nyuma yake ili apate huduma zote muhimu za matibabu,” ilieleza taarifa hiyo.
Kocha wa IBV Vestmannaeyjar, ameonyesha kusikitishwa na taarifa hizo huku akifichua mpango wa IBV kucheza mechi ya hisani kwa ajili ya kumchangia kipa huyo.