‘Maiti’ ya mmoja wa wana kikosi cha Operesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers, hivi karibuni iligomewa kupokelewa na wahudumu wa Mochwari ya Hospitali ya Wilaya ya Temeke jijini Dar baada ya wahusika hao kukataa rushwa, Amani lina stori kamili.
Hivi karibuni, OFM ilipokea malalamiko kutoka kwa raia wema kuwa, wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo wamekuwa wakipokea rushwa ili kulaza maiti kwa siri na pesa hizo huingia mifukoni mwao bila uongozi kujua.“Nyie watu wa OFM, hamna habari tu, pale mochwari ya Temeke kumekuwa na utaratibu wa ‘nyuma ya mlango’ yaani ukiwa na maiti yako kuingiza inawezekana tu. Unachotakiwa ni kuwa na pesa kidogo unawapoza kisha unawapa maiti wanakuhifadhia kwa siku utakazoamua mwenyewe.
“Mara nyingi wanalaza maiti kwa shilingi elfu hamsini mpaka laki moja kutegemea na siku ambazo maiti italala. Wengine wanaofanya hivi ni wale wanaotoa maiti mfano Lindi kupeleka Arusha, wanalaza pale, asubuhi yake wanaanza safari,” alisema raia huyo.
Baada ya kupata madai hayo, OFM ilijipanga na kuingia kazini kwa kutengeneza ‘maiti’ wao ambaye ni mmoja wa wana kikosi hicho, lengo likiwa kuona kama kuna ukweli wa madai hayo.
Baada ya kumtengeneza marehemu huyo, OFM walifunga safari hadi hospitalini hapo na kufika kwenye ofisi za watoa huduma wa mochwari na kumtoa mmoja wao pembeni ili kupanga naye dili la rushwa kabla ya kwenda kuleta ‘maiti’.
“Jamani, tunaomba msaada wenu, tumetokea Kibaha, Pwani, hapo kwenye gari tuna maiti ya ndugu yetu ambayo inatakiwa kulazwa katika mochwari yenu kwa siku mbili kabla ya kusafirishwa kwenda Mtwara, tafadhalini tunaomba msaada wenu na hapa tuna kiasi hichi cha pesa (OFM ikatoa shilingi elfu hamsini ili kumkabidhi).”
Hata hivyo, mhusika huyo alikataa katakata kupokea kiasi hicho cha pesa na kusema kuwa katika kitengo hicho hawajawahi kupokea mrungula kwa kulaza maiti hata kwa siku moja.
Baada ya kukataliwa hapo, OFM iliondoka eneo la tukio na kujiridhisha kuwa, hakuna mrungula wowote unaotolewa kwa kulaza maiti kwenye mochwari hiyo.
Huo ndiyo uadilifu unaotakiwa kwa watumishi wa umma na wa taasisi nyingine hasa katika utawala huu wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ ambaye kauli mbiu yake ni Hapa Kazi Tu!
-Gpl