Tuesday, April 26, 2016

Maiti ya Sangoma Yazua 'Timbwili' Mbeya...Yazikwa Ndani ya Nyumba yake Usiku

MBEYA

Mshtuko! Tofauti na utaratibu uliozoeleka, maiti ya aliyekuwa sangoma maarufu, Mzee Kalinga (80), mkazi wa Kijiji cha Chimala Muwale Wilaya ya Mbarali jijini hapa aliyeaga dunia akiwa na wake 15, watoto 102, wajukuuu 216 na vitukuu 16, imezikwa usiku ikiwa na masharti kibao.

Tukio hilo lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya sangoma huyo ambaye enzi za uhai wake alikuwa ni mganga wa kienyeji aliyetoa huduma ya kutibu maradhi kwa kutumia miti shamba.

Akizungumza na Wikienda, mmoja wa watoto wa marehemu, Shabani Kalinga alisema kuwa, baba yao alitoa maagizo kuwa siku akifa azikwe ndani ya nyumba yake majira ya saa 4:00 au saa 5:00 usiku na maiti yake ifunikwe kwa ngozi ya mnyama atakayechinjwa na nyama yake iliwe usiku.

Hata hivyo, Shabani, ndugu na jamaa wengine wa marehemu walidai kwamba walishindwa kumuuliza enzi za uhai wake ni kwa nini akifariki dunia azikwe kwa mtindo huo.

“Hata sisi tulipigwa na butwaa na kuamini pengine masharti hayo yalitokana na aina ya kazi ya uganga aliyokuwa akifanya,” alisema mmoja wa wanandugu hao.

Mashuhuda wa mazishi hayo walishangazwa na kitendo hicho cha sangoma huyo kuzikwa usiku kwani hawakuwahi kushuhudia msiba wenye masharti kama hayo.

Ukiachilia mbali kuzikwa usiku, pia alizikwa ndani ya nyumba yake na kuacha gumzo kijijini hapo.

SOURCE: GPL