Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanaia Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga mamaAnna kilango Malecela kuanzia leo.
Utenguzi huo umetokana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Anna kilango Malecela kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa jambo ambalo lilisababisha Ikulu kufanya uchunguzi wake na kubaini kuwepo kwa wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza na awamu ya pili ya uchunguzi bado inaendelea.
Akiongea Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akipokea hundi ya shilingi bilioni sita zilizotolewa na Ofisi ya Bunge baada ya kubana matumizi kwa ajili ya kununulia madawati, Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa sana na hali hiyo.
Amesema idadi ya wafanyakazi hewa mkoani Shinyanga huenda ikaongezeka zaidi kwani wilaya mbili za mkoa huo bado zinaendelea kuhakikiwa.
Rais pia ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul R. Dachi kwa kumshauri vibaya Mkuu wa Mkoa.
Mama Anna Kilango Malecela, ambaye katika awamu ya nne alikuwa Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi na Mbunge wa Same Mashairiki, anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kwanza kuachishwa kazi akiwa amedumu katika nafasi hiyo kwa mwezi mmoja tu..