Serikali imetoa Sh900 milioni kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu nchini. Fedha hizo zilitolewa katika kipindi cha Novemba mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema watu 21,634 waliugua ugonjwa huo na wengine 338 kufariki dunia tangu ulipolipuka Agosti 15 mwaka jana.
Kuongezeka kwa kasi ya kusambaa ugonjwa huo nchini na ongezeko la wagonjwa na vifo kulimfanya Rais John Magufuli kufuta sherehe za Uhuru (9 Desemba) na kuwataka wananchi wote akiwamo yeye kushiriki usafi wa maeneo yao ya kuishi kuepuka ugonjwa wa kipindupindu.
Alisema kuenea kwa ugonjwa huo nchini ni aibu kwa kuwa unatokana na uchafu ambao unaweza kusafishwa bila gharama yoyote.
Waziri Ummy alizungumzia mgawanyo wa fedha hizo kuwa Sh520 milioni ziligawanywa kwenye mikoa iliyoathirika na ugonjwa huo, Sh251.1 milioni zilitumiwa kununulia dawa na vitenganishi.
Alisema Sh328.8 milioni zilitumika kwa kamati za afya kitaifa na pia kutekeleza shughuli mbalimbali za uelimishaji jamii, mafunzo ya wataalamu wa afya na kuwapeleka katika mikoa ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo.
Waziri huyo alisema takwimu za mwezi uliopita zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa imepungua, sambamba na idadi ya mikoa na wilaya.
“Ifahamike kuwa maji na mazingira yetu bado yanaweza kutunza vimelea hawa wa kipindupindu na jitihada tulizojiwekea, nasisitiza ziwe endelevu kwa mikoa yote,” alisema Waziri Ummy.
“Ifahamike kuwa maji na mazingira yetu bado yanaweza kutunza vimelea hawa wa kipindupindu na jitihada tulizojiwekea, nasisitiza ziwe endelevu kwa mikoa yote,” alisema Waziri Ummy.