Ukatili uliofanywa na watu wasiojulikana wa kuwachinja watu wanane wa kitongoji cha Kibatini mkoani Tanga, umesababisha wakazi wa kitongoji hicho kuanza kuyahama makazi yao.
Watu hao walichinjwa usiku wa Mei 31 nje ya nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji hicho kwa madai kuwa walisababisha “vijana” wao kukamatwa na polisi baada ya kutoa taarifa zao wakati wakizurura kwenye eneo lao.
Waliouawa katika tukio hilo ni mwenyekiti huyo, Issa Hussein, kaka yake, Mkola Hussein, Hamis Issa, Issa Ramadhani na wengine wawili waliotambulika kwa jina moja la Kadir, Mikidadi na Salum.
Jana baada ya mazishi ya watu hao, mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk alipeleka lori aina ya Mitsubishi Fusso kwa ajili ya kuwahamisha wanakijiji hao.
Wakazi wayahama makazi
Diwani wa kata ya Mzizima, Fredrick Chiluba alisema wakazi wa Kibatini wameamua kuhamia kitongoji cha Kona-Z kilichopo kijiji jirani Kiomoni.
Mwandishi alishuhudia wakazi takriban 60 wa Kibatini wakitoa vyombo, huku wengine wakiezua mabati kwenye nyumba zao wakati wakisubiri gari ambalo baadaye liliwasili na kuwachukua.
“Wameingiwa na hofu ya kibinadamu na jambo hili lipo moyoni mwa mtu, hivyo huwezi kumng’ang’aniza kukaa hapo wakati anahisi hayupo salama,” alisema Chiluba.
Hadija Hussein alisema wameamua kuhama kwa sababu mara baada ya kukamilishwa kwa shughuli za mazishi ya ndugu zao wanne, ilipofika saa 6:00 usiku, askari waliokuwepo kwenye viwanja vya nyumba ya marehemu Mkola Hussein kulinda usalama hawakuonekana.
“Tulipatwa na wasiwasi mkubwa tulipoona askari na magari yao wameondoka, tukajua sasa na sisi tunakuja kuchinjwa.Hatukupata usingizi kwa hofu, ndipo asubuhi tukaamua kuondoa vyombo,” alisema.
Alisema mbunge alipokwenda kuwahani, walimuomba gari la kuhamisha vyombo vyao ili waondoke kabla jioni haijafika.
Mbunge Mbarouk alisema alipowasili eneo hilo na kukuta hakuna ulinzi, alimpigia simu mkuu wa polisi wa Wilaya ya Tanga ambaye alipeleka askari.
“Nilipowauliza viongozi wa Jeshi la Polisi waliniambia askari wapo wanafanya kazi ya kuzungukia maeneo, lakini haikuwa haki kuwaondoa askari mara tu baada ya kufanyika mazishi,” alisema Mbarouk.
Mbunge huyo alisema ameushauri uongozi wa polisi kupeleka ulinzi hata wanakohamia kwa sababu wauaji lazima watapata taarifa ya waliko na wanaweza kuwatendea chochote.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo alisema askari hawakuwa wameondoka kijijini hapo bali walikuwa wamefanya mbinu za kufanya doria maeneo yanayozunguka kitongoji hicho.
“Usiku huo kwenye kitongoji kulikuwa na kikosi maalumu cha FFU ambacho mimi mwenyewe nilikuwa nakiongoza usiku kucha. Tulikuwa tukifuatilia maficho ya wahalifu, kitaalamu tunaita undercover,” alisema.
Kamanda huyo alisema wakati polisi ikiendelea na operesheni, si vyema kuwatisha wananchi kwa kuwa tangu yalipofanyika mauaji hayo, askari hawajaondoka.
RC: Mauaji ya Tanga si ugaidi
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amesema mauaji yanayotokea katika mitaa ya jijini Tanga na Amboni si vitendo vya kigaidi, bali yanatendwa na kundi la watu wanaotaka kuvuruga amani.
Amesema hii ni vita ya kiuchumi inahusiana na ujio wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga na kwamba Serikali itahakikisha inawakamata waliohusika.
Alisema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza pamoja na vyama vya siasa vya wa wilayani humo.
Shigela, ambaye alikuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza kupokea taarifa ya maendeleo ya kabla ya kuanza ziara wilayani humo, alisema Serikali haiwezi kukubali kuona kundi la watu wachache wanaharibu amani iliyopo.