Sunday, May 18, 2014

Walimu washauriwa kuacha kutumia VIROBA wakati wa kufundisha..SOMA ZAIDI

OFISA Elimu Mkoa wa Pwani Yusufu Kipengele amewataka walimu mkoani humo kuachana na tabia ya kutumia vilevi waingiapo madarasani kufundisha kwani hali hiyo inachangia kushuka kwa kiwango cha elimu.
Imebainika kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakitumia vilevi aina ya viroba kabla ya kuingia madarasani kufundisha hali ambayo ni moja ya sababu ya kiwango cha elimu kushuka ambapo mwalimu husika kufundisha chini ya kiwango.
Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati akifungua kikao cha umoja wa walimu wakuu wa shule za sekondari Tanzania (TAHOSSA) kanda ya Mashariki na kusema kuwa tabia kama hiyo haipaswi kufumbiwa macho na viongozi wa idara ya elimu ili kurekebisha mwenendo wa walimu.
Picha ya pamoja na baadhi ya walimu wakuu wanaounda umoja wao wa TAHOSSA Kanda ya mashariki.
Picha ya pamoja na baadhi ya walimu wakuu wanaounda umoja wao wa TAHOSSA Kanda ya mashariki.
“Baadhi ya walimu wamekuwa wakitumia pombe aina ya viroba jambo ambalo limekuwa likichangia maadili kuvunjika kwa walimu na wanafunzi wanaowafundisha,” alisema Kipengele.
Alisema kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakitumia vilevi hivyo pamoja na wanafunzi hivyo kufanya taaluma kushuka kwani walimu hao uwezo wao unashuka na kushindwa kuwapatia kile wanachotakiwa kuwafundisha wanafunzi.
Akijibu baadhi ya hoja ikiwemo ya kukosa fedha kwa ajili ya wasimamizi wa mitihani ya vitendo aliwataka kuhakikisha wanapeleka suala hilo kwenye uongozi wa bodi ili waridhie ili wazazi wachangie sehemu ya gharama hizo ambapo kwa upande wa serikali nayo itachangia kwa kiasi.
Awali akimkraibisha mgeni rasmi ambaye ni ofisa elimu wa mkoa mwenyekiti wa TAHOSSA Omary Msami alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubw aikiwa ni pamoja na mitihani ya vitendo kutokuwa na fedha toka wizarani.
“Tunaomba tupatiwe mafunzo kazini kwani walimu hawapatiwi jambo ambalo linasababisha walimu kushindwa kwenda na wakati kwani baadhi ya mambo ya ufundishaji yamekuwa yakibadilika,” alisema Msami.
Aidha aliomba ukaguzi mashuleni ufanywe kila mwaka ama baada ya miaka miwili ili kurekebisha kasoro zinazojitokeza na kuwalipia wakaguzi hao ili kuzipunguzia mizigo shule.
Umoja huo unaundwa na mikoa ya Pwani na Morogoro ambapo kuna jumla ya shule 384 na walimu wakuu 131.