Thursday, July 17, 2014

CHEKA KISHAROBARO: SHEHHE AGAWA MBUZI AKIZANI NI MBWA....... SHARE

Mzee mmoja wa kiislam maeneo ya Kibaha alikuwa anaenda katika mnada kununua mbuzi kwa ajili ya kitoeo cha siku kuu ya Idi. Vijana wa kihuni wa mtaani walipojua kuwa anaenda
kununua mbuzi waka panga njama wamuibie. Wakajikusanya kama sita hivi kisha wawili wakaenda kukaa maeneo ya sokoni, wawili wakakaa njiani katikati ya sokoni na nyumbani kwake, na wawili wakamsubiri mitaa miwili kabla ya kufika nyumbani kwake.
Yule mzee akiwa na kanzu yake na msuli akanunua mbuzi wake na kumfunga kamba shingoni na kuanza kurudi nae nyumbani. Alipotoka tu sokoni akaona vijana wawili wananunua kuku, wale vijana wakamsalimia
Vijana: Shikamoo mzee
Mzee: Marahaba wajukuu zangu
Vijana: (kwa mshangao kidogo) mzee! Mbona umenunua mbwa sikuku yote hii? wa nini?
Mzee: Sio mbwa huyu ni mbuzi, watoto wadogo mshapofuka macho.
Vijana: mzee angalia asikung’ate.
Wale vijana wakaendelea na shughuli zao. Mzee akashangaa kidogo kisha akamuangalia mbuzi wake, akatikisa kichwa kwa kusikitika akiwasikitikia wale vijana.
Akaenda alipofika katikati ya njia akakutana na vijana wawili wakitokea kule anapoelekea yule mzee. Wale vijana walikuwa wamesimama njiani wanaangalia kitu katika simu hivyo walikuwa hawamuoni anayekuja yule mzee alipowakaribia wale vijana wakaruka kwa
mshtuko na kusogea pembeni kwa ghafla huku wakiambiana
Kijana 1: Mbwa huyo atakung’ata…
Kijana 2: Nilikuwa sijamuona, yaani nimeponea chupuchupu.
Kijana 1: babu huyo mbwa si atakutia najisi? Kwa nini usimtupe?
Yule mzee akmuangalia mbuzi wake kwa makini kisha akaanza kuwa na wasi wasi. Akaanza kuhisi kama amechanganyikiwa maana watu wa kwanza walimuambia ni mbwa na watu wa pili wengine nao wanasema hivyo hivyo. Akawa anaenda nambuzi wake lakini huku anamuangalia.
Akafika njiani akachukua bakora akamchapa mbuzi wake ili asikie ataliaje, yule mbuzi akalia “meeeee”, akajisemea moyoni. “bwanaee! Huyu ni mbuzi wale vijana ndo watakuwa wamechanganyikiwa”
Alipofika mbele akakutana na vijana wengine wanatokea mbele yake
Vijana: mama yangu weeee! Dunia imeisha, hata wewe unabeba mbwa, shehe mzima na kanzu safi, siku ya sikukuu. He! Huoni aibu mzee mtaani watu wanakuheshimu mtu wa dini safi lakini unanunua mbwa ufuge.
Mzee: (akajitetea huku akiwa hajiamini)jamani huyu ni mbuzi sio mbwa tena analia meee ukimpiga
Kijana mmoja akachukua jiwe akampiga nalo mbuzi, mbuzi akalia “meee”, wale kijana wakajifanya kushtuka na kurudi nyuma, “he! Tena anabweka kama mbwa wa polisi, hebu lete tukusaidie tukamtupe mbali maana atakuja kung’ata watu hapa mtani.
Mzee akaanza kuamini kuwa huenda yeye ndiye anamatatizo ya akili na huenda ameuziwa mbwa kweli, akawapa wale vijana yule mbuzi na kuwaambia “kamtupeni mbali maana asije kututia najisi hapa na kutung’ata”
Vijana wakamchukua mbuzi na kutimua nae kwenda kusheherekea sikukuu