Saturday, August 30, 2014
MAITI YA MWANAMKE YAZUA KIZAA ZAA GEITA,YAZIKWA KI- EBOLA EBOLA
Maiti ya mwanamke mmoja Bertha Boniphace(23)mkazi wa kijiji cha Katoro Kata ya Katoro Wilaya na Mkoa wa Geita mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola imeutikisa mji wa Geita kiasi cha wakazi wa mji huo kuhofia kushikana mikono wakihofia kuambukizwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya mwanamke huyo kufariki dunia akiwa katika hospitali ya Wilaya ya Geita na ndugu kunyimwa mwili wake kwenda kuuzika na badala yake mwili huo kuzikwa na Serikali.
Baada ya serikali kugoma kutoa mwili wa mwanamke huyo kwa ndugu zake ili wakauzike,mvutano mkali ulitokea kati ya Uongozi wa Hospitali ya wilaya ya Geita,na ndugu wa marehemu huyo ndugu hao wakipinga mwili wa marehemu kwenda kuzikwa na serikali bila kutoa heshima zao za mwisho.
Kufuatia hali hiyo walinzi wa Hospitali waliamuliwa kuwaondoa eneo hilo ndugu wa Marehemu waliokuwa wamefurika wakitaka kujua sababu ya wao kuzuiliwa kuona mwili wa marehemu bila kupewa taarifa sahihi za ugonjwa uliosababisha kifo cha ndugu yao.
Nusura walinzi na ndugu wa marehemu warushiane ngumi na watu hao ambao walikuwa wamefura hasira na baadaye walinzi hao ambao hawakuwa na siraha waliamua kuokota mawe na kuanza kuwarushia ndugu wa marehemu hali iliyosababisha ndugu wa marehemu kutimua mbio.
Baadaye mwili wa marehemu ulitolewa kwenye Chumba maalumu cha hospitalini hapo kwenda kuzikwa na halmashauri ya Geita.
Msafara wa kwenda kuzikwa kwa mwili wa marehemu katika Makaburi ya Mkoani Mjini Geita uliongonzwa na mganga mkuu wa wilaya ya Geita,Dk.Noel Makuza aliyeambatana na watalaam wengine waliovalia mavazi maalum ya kuzua magonjwa ya kuambukiza.
Mgonjwa huyo alifariki usiku wa kuamkia juzi kutokana na kusumbuliwa na tatizo la Kuharisha na Kutapika damu pamoja na kutokwa na damu puani hali ambayo ilisababisha hofu kubwa na baadhi ya wakazi wa mji wa Geita walianza kuvumisha kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola na kuanza kusambaza ujumbe mfupi kwenye simu za mkononi kuchukua tahadhali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Geita,Dk.Adamu Sijaona alisema hakuna mgonjwa wa Ebola aliyefikishwa Hospitalini hapo na kudai kwamba dalili za Ebola zinafahamika.
“Mgonjwa huyu ,tumekaa nae kwa siku 10 alikuwa na tatizo la Madonda ya Tumbo na alikuwa akitokwa damu puani na ukeni lakini haijathibitishwa kama ni ebola au la ,isipokuwa dalili za Ebola zinashabihiana na dalili za magonjwa mengine kama Homa ya Bonde la Ufa,na mengine”alisema Dk.Sijaona.
Alisema Vipimo vya mgonjwa huyo vimechukuliwa kwenda kwa mganga mkuu Taifa kwa vipimo zaidi ili kujua kama alikuwa anasumbuliwa na Ugonjwa huo wa Ebola kutokana na Hospitali hiyo kutokuwa na vipimo vya kubaini ugonjwa huo.
Akizungumzia suala la ndugu kuzuiliwa kuona mwili wa marehemu na mwili huo kwenda kuzikwa na Halmashauri badala ya ndugu, Dk.Sijaona alisema”Tulifanya hivyo kwa kuwa tulikuwa na wasiwasi kwa sababu mgonjwa huyo alihisiwa mwenye dalili za Ugonjwa wa Ebola,lakini tulichukua ndugu wawili wakaoenda kuona alipozikwa ndugu yao.”alisema Daktari huyo.
Hata hivyo mmoja wa ndugu wa marehemu,Mariam Boniphace alisema mdogo wake alianza kuugua Agosti 19,mwaka huu kwa kutapika na kuharisha kawaida alipopimwa alionekana anasumbuliwa na Malaria lakini baada ya siku tatu alianza kutapika na kuharisha damu na damu nyingine ilikuwa inatokea puani na sehemu za siri.
“Tunamashaka yawezekana kuwa ni Ebola,kwa nini madakt ari wametuzuia kuaga mwili wa marehemu wala kumgusa?,na bado wamedai wamechukua vipimo na kuvipeleka nchi za nje kwa uchunguzi zaidi na majibu wamesema baada ya wiki moja yatapatikana”
Katika hatua nyingine Dk.Sijaona amewatoa wasiwasi kwamba Geita hakuna mgonjwa wa Ebola na badala yake amewataka wananchi kuchukua tahadhali kubwa kuhusu ugonjwa huo wanapoona dalili kama hizo kutoa taarifa mapema ikiwa ni pamoja na kumpeleka mgonjwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.