Saturday, August 16, 2014

TP MAZEMBE WAKIMBIA NCHI KWENDA ZAMBIA KUJIANDAA NA ‘MECHI YA KUFA MTU’ DHIDI YA MAHASIMU WAO WAKUBWA AS VITA WIKI IJAYO

KLABU ya TP Mazembe imetua Ndola, Zambia kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa mwisho wa Kundi A, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mahasimu wao wakubwa, AS Vita, zote za Jamhuri ya Kidemokasia ya Kongo (DRC).
Vita wataikaribisha Mazembe mjini Kinshasa Oktoba 22 katika mchezo wa mwisho, timu zote zikiwa zimetinga Nusu Fainali, lakini zitakuwa zinapigania kuongoza kundi hilo.
Siku hiyo, CS Sfaxien ya Tunisia itamenyana na ES Setif ya Algeria katika mchezo wa Kundi B. Oktoba 24, Al Hilal ya Sudan itaikaribisha Zamalek ya Misri katika mchezo mwingine wa Kundi A kukamilisha ratiba, wakati Esperance ya Tunisia itakuwa mwenyeji wa Al Ahly Benghazi ya Libya katika mchezo wa Kundi B.

Mbwana Samatta baada ya kuwasili na Mazembe mjini Ndola jana

Mazembe waliwasili jana kwa basi lao kubwa Mercedes "Pullman" baada ya safari ya tangu saa 2:30 asubuhi hadi saa 11:30 jioni tayari kwa kambi ya siku sita ya kujiandaa na mchezo ambao inaaminika siku hiyo DRC nzima itasimama kuupisha mtanange huo. 
Washambuliaji wote wa Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wamewasili na timu yao Ndola wakiwa fiti kabisa na leo wameanza mazoezi baada ya jana kupumzika kwa uchovu wa safari.
Timu zote zina pointi 10 baada ya mechi tano, lakini Mazembe wanaizidi Vita bao moja katika wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. Vita iliifunga Zamalek kwake, Misri 1-0 katika mchezo uliopita siku chache baada ya Mazembe kutoa sare na Waarabu hao mjini Cairo.

Thomas Ulimwengu kushoto na Robert Kidiaba kulia baada ya kuwasili Ndola 

Mchezo wa kwanza Lubumbashi baina ya vigogo hao wa DRC, Mazembe iliifunga Vita 1-0 Mei 25, mwaka huu na katika mechi za Ligi Kuu ya DRC, Mei 23 Mazembe iliifumua Vita 4-1 Lubumbashi, ziliporudiana Mei 11, mwaka huu ikashinda tena 1-0 Kinshasa.
Lakini AS Vita inaonekana kuimarika zaidi hivi sasa na inataka sana kufuta uteja wao kwa wapinzani wao hao- na bila shaka kwa kulijua hilo, Mazembe wamekimbia nchi kwa maandalizi.