Monday, September 22, 2014

HASARA KWA MTOTO KUDEKEZWA...!


Ni siku nyingine wajukuu zangu yenye baraka na neema, kwasababu tumekutana tena na kujadili mambo mazuri, lengo likiwa kufahamishana na kuelekezana mambo mema.
 
Kama utakuwa mwerevu kama yule rafiki yako au zaidi ya yeye utakuwa umesoma kichwa cha habari hapo juu na kutambua mada yetu ya leo.
 
Kama hujaelewa usijali nitakufafanulia kwa kina, ili uweze kuelewa nini nataka tujadili leo.
 
Ni kawaida kusikia watoto wenzenu wakisema mtoto fulani anadekezwa sana na wazazi wake mpaka anakuwa mjinga! Lakini wengi wenu hamfahamu nini sababu ya mtoto huyo kudekezwa na hao wazazi wake.
 
Kudekezwa ni hali ya mtoto kulelewa bila kukanywa jambo hata likiwa baya na wazazi au walezi wake wakiamini kufanya hivyo ndio kumpenda mtoto.
 
Zipo hasara nyingi ambazo atazipata mtoto anayedekezwa, hasara ya kwanza ambayo iko wazi mtoto huyo ni lazima atakuwa na tabia mbaya kwani hajawahi kukatazwa jambo baya. Anaweza akawatusi wakubwa zake asijue kuwa ni tabia mbaya kwani hakuwahi kukanywa kuwa kutukana ni tabia mbaya.
 
Pia, anaweza kuwa mtovu wa nidhamu wa hali ya juu hata kufikia hatua ya kuwaaibisha wazazi wake mbele za wageni.
 
Mfano wapo baadhi ya watoto wanaodekezwa wakienda ugenini utawasikia wakisema,“chakula chenu kibaya mama mimi sitaki kula aaaah” Hizo ni baadhi ya kauli za watoto wanaodekezwa na kukosa heshima.
 
Ni vizuri wazazi mkawafundisha maadili mazuri watoto, badala ya kuwadekeza na kushindwa kuwakanya pindi watakapokosea jambo.
 
Kuwapenda watoto si kuwadekeza, badala yake mnawaharibu watoto kwa sababu hawakanywi wanapokosea na kujikuta wanakuwa na tabia mbaya.
 
Naaamini wajukuu zangu wote mtakataa tabia ya kudekezwa ili muweze kukanywa mnapokosea ili muwe na tabia njema