Tuesday, September 16, 2014

Okwi wa kazi gani? mashabiki wa Yanga wakejeli


STRAIKA mpya Mbrazili aliyekuwa akikejeliwa na mashabiki wa Yanga, Genilson Santos ‘Jaja’ jana Jumapili amepiga bao mbili kati ya tatu zilizoipa ushindi timu yake dhidi ya Azam na kushangilia kwa ishara ambazo mashabiki walizitafsiri kwamba alikuwa akiwauliza; “Okwi wa kazi gani Yanga?”
Awali kabla ya dirisha la usajili halijafungwa kulikuwepo na mzozo baina ya Kocha Marcio Maximo na uongozi wa timu uliotaka straika aliyejiunga na Simba, Emmanuel Okwi abaki Yanga na Jaja akatwe kwa madai kwamba ni mzito na hayuko fiti kama Okwi aliyelipwa fedha nyingi.
Lakini Maximo akashikilia msimamo wake kwamba Jaja ndiye chaguo lake na Okwi hatacheza Yanga kutokana na utovu wa nidhamu na kususa mara kwa mara.Licha ya kuwathibitishia Yanga kwamba yeye ni mashine na amesajiliwa kwa ajili ya kufunga tu, Jaja jana aliwaziba midomo mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakimzomea siku za nyuma kwa madai kwamba ni mzito na hana lolote.
Katika mchezo huo wa Ngao ya Hisani uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa huku kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ akidaka kwa mbwembwe na sarakasi kuwakejeli Azam ambao walimtema, Jaja alipiga mabao mawili katika dakika za 56 na 65. Bao la tatu lilifungwa na Simon Msuva aliyeingia kuchukua nafasi ya Nizar Khalfan katika dakika ya 87.
Kwenye bao la kwanza, Mbrazil huyo aliunganisha mpira wa kisigino ikiwa ni pasi ya Msuva ambayo ilitokea kwa Haruna Niyonzima wakati bao lake la pili aliudokoa mpira baada ya kupokea pasi ya Khalfan Ngassa. Msuva alipachika bao lake kwa kumalizia pasi ya Hussein Javu aliyetokea jirani kabisa na katikati ya uwanja.
Makocha wote wawili Joseph Omog wa Azam na Maximo wa Yanga ambao ndio wanaoongoza idadi ya mabosi wanaolipwa zaidi nchini, walifanya mabadiliko katika vikosi vyao lakini yale ya Azam hayakuisaidia kwani ilikosa mipango kwenye boksi la Yanga ingawa idara nyingine ilikuwa vizuri.
Dakika ya pili, David Mwantika aliumia mpira ukasimama lakini dakika ya sita Yanga ilifanya shambulizi kali langoni mwa Azam ambapo Ngassa alipiga krosi nzuri lakini umaliziaji ulikuwa mbovu.
Mshambuliaji wa Azam Mrundi Didier Kavumbagu aliyechezea Yanga msimu uliopita alishindwa kuunganisha kwa kichwa krosi safi ya Erasto Nyoni katika dakika ya tisa, Jaja licha ya kufunga lakini mara kadhaa alishindwa kuendana na kasi ya Ngassa, hivyo kumfanya awe anamsubiri kila muda wakati huo mabeki wa Azam wakirudi kumkaba.
Dakika ya 14, Kipre Tchetche alipaisha mpira na kushindwa kuunga krosi ya Kavumbagu lakini Yanga nayo ilijibu mapigo dakika ya 18 ingawa Haruna Niyonzima alishindwa kumalizia mpira uliokolewa na mabeki wa Azam.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Simon Mbelwa wa Pwani, baada ya kumalizika kwa dakika 54 za mwanzo, Ngassa na Sure Boy walibadilishana jezi ikiwa ni ishara ya kwamba soka si mchezo wa ugomvi.
Mmoja wa maofisa wa Yanga akizungumzia tukio hilo alisema; “Tunazo jezi nyingi kama hizi na kuna seti ambazo tumekuja nazo hapa uwanjani.”
Zoezi la ukataji wa tiketi za kieletroniki lilionekana kuwa gumu kwani mashabiki walitumia muda mrefu kukata tiketi na hivyo kuleta usumbufu.Azam FC: Mwadini Ali, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni/Gadiel Michael, David Mwantika, Aggrey Moris, Bolou Michael, Himid Mao/Khamis Mcha, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche/Ismail Diara na Leonel Saint Preux/Kelvin Friday.
Yanga: Dida, Said Juma/Hassan Dilunga, Oscar Joshua, Cannavaro, Kelvin Yondani, Twite, Said Juma, Niyonzima/Kiiza, Jaja/Javu, Ngassa/Omega Seme na Nizar/ Msuva.
-Mwanasport