Tuesday, September 2, 2014

SAKATA LA KIFO CHA KAMANDA BARLOW, MKEWE MBARONI MAPYA YAIBUKA

Sakata la madai kuwa mke wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, Stella Barlow (pichani)alitimuliwa ukweni kwa mapanga limechukua sura mpya baada ya ndugu wa mumewe kuibuka na kutoa ufafanuzi.
Mjane Stell Barlow wakati wa mazishi ya aliyekuwa mume wake, Kamanda Liberatus Barlow.
 Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki iliyopita, ndugu wa marehemu Kamanda Barlow, aliyejitambulisha kwa jina moja la Lyimo alisema si kweli hata kidogo kuwa walimkimbiza kwa mapanga shemeji yao huyo.

“Kilichotokea ni kwamba tulimuambia huyo mama kuwa hawezi kufanya chochote kwenye kaburi la mumewe mpaka akamuone kiongozi wa ukoo. Kimila tangu wakati kaburi linachimbwa, linakuwa chini ya uangalizi wa wanaume na hata baada ya kuzika haliwezi kuwa chini ya mwanamke, hilo tulimjulisha,” alisema Lyimo.
Kamanda Barlow enzi za uhai wake.
 Alifafanua kuwa wamewahi kufanya misa ya kumuombea marehemu Barlow na ndugu wengine na mama huyo aliarifiwa lakini hakuja. “Ujumbe wetu ni kwamba muambieni huyo mama  kuwa siyo vizuri kuchafua ukoo kwa sababu hatuna ugomvi naye na hakika kama ni wa kulaumiwa ni yeye siyo sisi wana ukoo,” alisema Lyimo.
 Wakati huo huo, kwenye Gazeti la Uwazi la Agosti 27 mwaka huu tuliweka kimakosa picha ya mke wa marehemu Kamanda James Kombe badala ya mke wa kamanda marehemu Liberatus Barlow, Stella Barlow. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata wahusika- Mhariri.