Tuesday, September 23, 2014

SERIKALI ZAWAONYESHEA KIDOLE TAASISI ZINAZOFANYA KAZI YA UDALALI KWA KUKUSANYA VIJANA WA KITANZANIA KUJIUNGA NA KUNDI LA KIGAIDI LA AL SHABAAB LA SOMALIA.


WAKATI Serikali ikipambana na vitendo vya kigaidi nchini, imebainika kuwa baadhi ya taasisi zilizosajiliwa kisheria nchini zimekuwa zikifanya kinyume cha sheria `udalali’ wa kuwapeleka vijana wa Kitanzania kujiunga na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Shaabab nchini Somalia ambako wameishia kupata matatizo, ikiwa pamoja na kupoteza maisha. 

Kutokana na hali hiyo, wameaswa kutokubali kurubuniwa, na badala yake wawe na uzalendo kwa nchi yao na pia kujikita katika kufanya shughuli halali, badala ya kukimbilia nje ya nchi wanakoishia kuingizwa katika makundi hatari, yakiwemo ya kigaidi na yale ya mtandao wa wauza dawa za kulevya.

Aidha, wamesisitizwa wavitumie `vijiwe’ katika kuunganisha nguvu za kujiendeleza kiuchumi, na si kuvigeuza mahali pa kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.

Hayo yalibainishwa jana na aliyekuwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Somalia, Balozi Augustine Mahiga na Mkuu wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol Tanzania), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustavus Babile.

Wakizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani mkoani hapa jana, ambapo kulikuwa na mdahalo wa vijana kuhusu kaulimbiu ya siku hiyo;

‘Haki ya Watu Wote Katika Amani’, viongozi hao waliweka wazi kuwa vijana wa Tanzania, bila kujijua wanayaweka rehani maisha yao huku wakiichafua nchi yao yenye heshima kubwa duniani. Al Shabaab Balozi Mahiga alisema alipokuwa Somalia, aliambiwa kuwa kuna Watanzania wanapigana kusaidia kundi hilo la kigaidi la Al-Shabaab na alishuhudia baadhi ya maiti za vijana hao waliouawa katika mapigano ya Serikali ya nchi hiyo na kundi hilo.

Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, alipata nafasi ya kuzungumza na mmoja wa vijana walio katika kundi hilo, akamwambia kwamba alikwenda kujiunga na kundi hilo baada ya kurubuniwa kuwa watapata fedha nyingi.

“Wanasema waliambiwa kuwa kama wakitoka hai, basi watakuwa wamepata fedha lakini wakifa, familia zao zitanufaika…lakini wakasema wanaishia kwenye vifo na kufungwa bila kupata faida waliyoikusudia.

“Wakati nikiwa pale, maofisa wa Somalia wakati mwingine walikuwa wananiambia kabisa ‘tumetoka kumaliza vijana wako’, alisema Balozi Mahiga.

Mbali na vijana hao wanaopigana na waliouawa, Balozi Mahiga alisema pia kuna vijana wengine ambao wamekamatwa wakiwa katika kundi hilo na wamefungwa katika Magereza ya nchi hiyo.

Ukiacha vijana walio Somalia, Balozi Mahiga alisema pia kuna vijana wamekwenda nchini Yemen kujiunga na vikundi hivyo vya kigaidi, lakini kutokana na kutokuwa na mafunzo imara wanaishia kukamatwa na kufungwa au kuuawa, huku akibainisha kuwa Al- Shabaab ndio waliotoa mafunzo na wanaendelea kuyatoa kwa kundi la kigaidi la Nigeria la Boko Haram.

Alisema ana imani kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini na alishatoa taarifa kwa Serikali, ambapo alikuta vyombo hivyo vya ulinzi na usalama pia wanajua kuwa kuna vijana wanarubuniwa kwenda kujiunga na makundi hayo.

Naye Kamishna Babile, alikiri kuwa ni kweli kuna vijana wamekamatwa katika nchi hiyo kutoka katika kundi hilo la kigaidi ambao ni Watanzania. Alisema Polisi nchini ilifuatilia nchini humo na kubaini kuwa vijana hao wana hati za kusafiria za Tanzania zilizotolewa Zanzibar.

“Unajua kila Mtanzania ana haki ya kuwa na hati ya kusafiria, tatizo ni anaposafiri hatujui anakwenda kufanya nini,” alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kubaini kuwa hati hizo zilitolewa Zanzibar, Polisi ilifuatiliwa mpaka kwa wazazi wa vijana hao na kuwapata.

Kwa mujibu wa Kamishna Babile, wazazi hao walipoulizwa namna vijana hao walivyoondoka nchini, walijibu kwamba walitoroka.

Aliongeza kuwa uchunguzi zaidi ulibaini kuna taasisi zimesajiliwa nchini kwa ajili ya kufanya kazi fulani zinazokubalika kisheria, lakini taasisi hizo hazifanyi kazi walizojisajili nazo.

Taasisi hizo kwa maelezo ya Kamishna Babile, zimekuwa zikiandikisha vijana na kusaidia kuwasafirisha kwenda katika vikundi hivyo, ambako hupatiwa mafunzo na kugeuzwa kuwa vijana wenye siasa kali za kidini, walio tayari kwa lolote ikiwemo kujitoa mhanga.

Hayo yameibuka wakati Serikali, kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwa imetangaza kuanza kuhakiki wa vyama vya kijamii zaidi ya 9,550, vikiwemo 956 vya kidini, ili kuboresha huduma zinazotolewa na vyama hivyo nchini tangu kuanzishwa kwake na kwamba, vitakavyoonekana kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa, vitafutwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isack Nantanga alisema kazi hiyo itaanza mwezi ujao ambapo pamoja na mambo mengine, kazi hiyo inalenga kuvifuta kutoka katika daftari la Msajili vya Vyama vya Kijamii vyama ambavyo vitabainika kuwa havina sifa tena ya kuendelea kuwa katika daftari hilo.

Alisema vigezo ambavyo vinaweza kusababisha chama kufutwa kutoka katika Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii ni pamoja na kubainika kufanya shughuli tofauti na zile zilizoandikishwa katika Katiba ya chama hicho, kutolipa ada za mwaka kwa wakati na kutowasilisha kwa Msajili, taarifa za kila mwaka za utendaji kazi na mapato na matumizi ya fedha za chama husika.

Kamishna Babile alisema mbali na vijana wa Tanzania kushiriki katika makundi ya kigaidi, lakini hata katika biashara ya dawa za kulevya, hali ni mbaya.

Alitoa mfano wa mkutano wa mwaka jana wa dunia wa Shirika la Interpol ambao alihudhuria, kwamba aliitwa pembeni na kuoneshwa takwimu za matukio ya dawa za kulevya yanayowagusa vijana wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Kamishna Babile, takwimu hizo zilionesha kuwa katika matukio 50 yaliyohusu biashara hiyo haramu duniani yaliyokamatwa miezi mitatu kabla ya mkutano huo, vijana wa Tanzania walihusika katika matukio 30.

Mbali na takwimu hizo za dunia, Kamishna Babile alisema pia katika mkutano wa Interpol kwa nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), takwimu za eneo hilo pia zilionesha katika matukio 50 yaliyokamatwa ya biashara hiyo, matukio 30 yaliwahusu vijana wa Tanzania.

Ofisa huyo wa ngazi za juu wa Polisi, alisema ndio maana walianzisha Polisi Jamii, ambayo inaendeshwa na askari vijana wenye uwezo wa kuelewa vijana wenzao ili kuwaepusha katika matendo hayo.

Alifafanua kuwa katika Polisi Jamii, kuna programu 19 zinazohusu vijana, ikiwemo ya michezo inayolenga kumfanya kijana akose muda wa kwenda kujihusisha na makundi hayo.

Programu nyingine, alisema ni ya Usalama Kipaumbele cha Wote, ambayo inafundishwa katika shule mbalimbali nchini, lengo lake likiwa kuwafundisha vijana tangu wadogo shuleni ubaya wa kushiriki katika uhalifu.

Pia ipo programu ya Vijana wa Vijiweni, ambayo alisema inalenga kuwatoa katika vijiwe na kuwaweka katika maeneo ambako watajishughulisha na kazi ambazo ni endelevu.

“Tunataka hii Polisi Jamii iwe sehemu ya kila mmoja wetu,” alisisitiza Kamishna Babile.

Katika mdahalo huo, kuliibuka hoja ya kuhusisha dini ya Uislamu na ugaidi, ambapo Balozi Mahiga alisema suala hilo lilitokana na propaganda iliyoanza baada ya Marekani kupigwa katika tukio la Septemba 11, 2001. Alisema lilikuwa kosa kubwa kuhusisha Uislamu na ugaidi baada ya tukio hilo.

Akifafanua zaidi alitoa mfano wa Mashehe wa Uingereza ambao jana walitoa tamko la kusihi kundi la kigaidi la ISIS lililopo Iraq, lisimkate kichwa mfanyakazi wa kujitolea anayetoa huduma za kibinadamu nchini humo.

Pia alitoa mfano wa Somalia, ambako alisema Waislamu ni asilimia 99 kama si 100, lakini wanauawa na Waislamu wenzao wa Al-Shabaab, ambao wanaamini kuwa wao ndio wenye itikadi sahihi ya Uislamu.

“Wanazuoni wanapinga hili la baadhi ya watu kudhani wao ndio wanajua dini zaidi, naweza kusema hawa magaidi wamechepuka katika njia kuu ya dini, ambayo inataka amani na watu wote na kuanza kuua wenzao,” alisema.

Akizungumzia suala la kuchanganya dini na ugaidi, Kamishna Babile alisema matukio yote ya uhalifu nchini yanafanywa na Wakristo, Waislamu na Wapagani. Aliwataka washiriki wa mkutano huo waliohoji kuhusu Mashehe kutoka Zanzibar kushitakiwa Kisutu kwa ugaidi kuwa wasiangaliwe kwa dini zao, bali kwa uhalifu wanaoshitakiwa nao