Tukio lililodhihirisha kuwa wawili hao hawaivi, lilichukua nafasi juzikati katika Viwanja vya Leaders Club vilivyopo Kinondoni jijini Dar, kulipokuwa na uzinduzi wa filamu iliyokwenda kwa jina la Mateso Yangu Ughaibuni.
Wakati shamrashamra za uzinduzi zikiendelea, paparazi wetu aliwashuhudia wawili hao wakiombwa wapige picha kwa pamoja ambapo hakuna aliyekuwa tayari kutimiza zoezi hilo, wakachengana kwa kila mmoja kuchukua njia yake.
Wakizungumza na paparazi wetu, baadhi ya mastaa walioshuhudia kituko hicho, walisema Steve Nyerere na Mtitu wanatakiwa wakae pamoja wamalize tofauti zao hata kama mmoja wao hatorudi katika kiti chake cha uongozi lakini kwa heshima waliyojijengea katika tasnia ya filamu hawapaswi kuwa na mabifu.
“Sasa hawa ndio nini wanachokifanya? Wanaombwa kupiga picha ya pamoja kila mtu anatoa sababu zake lakini sidhani hizo sekunde kadhaa za kupiga picha zinaweza kuharibu ratiba zao,” alisikika muigizaji mmoja hivi maarufu.Baada ya kupata maelezo hayo kutoka kwa muigizaji huyo aliyeomba hifadhi ya jina, paparazi alimvaa Mtitu na kumuuliza kulikoni kugoma kupiga picha na mwenyekiti wake ambapo alijibu kuwa hakujua kama anatakiwa kufanya hivyo.
“Siwezi kugoma hata siku moja kwani mimi nina uhuru wangu vilevile sikujua kama wapiga picha wanataka picha yetu ya pamoja,” alisema Mtitu.Kwa upande wake Steve, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alijibu kwa mkato akionesha kulipuuza.“Achana na hayo mambo kuna mengi ya kufanya,” alisema Steve Nyerere.