Sunday, October 26, 2014

FREEMASON YAZUA KIZAAZAA KWENYE ZOEZI LA CHANJO HUKO RUFIJI PWANI

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgCHxk0fLxNOfi1ppzNbB5ghgycbLrqCt5593ErMg4MJhRkmlJ02xp6mnQXvGo8qeXUN2O6OGJ9TO1puqu43ryOKqWk2wrizGQX23hE0nqxKc7voo9oPRh0sY9xgtZD5k5C9WWpoRNNtkU-/s1600/elkra.JPG

Chanjo ya surua na rubella katika baadhi ya maeneo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani imekumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ya baadhi ya wananchi kugoma kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kwa madai kuwa dawa hizo zinatolewa na ‘Freemason’ ili kuwafunga vizazi
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Rufiji, Michael Mollel alisema jana kuwa uvumi huo upo katika kata za Mgomba na Mlanzi.


Alisema mahudhurio ya wananchi katika vituo vya chanjo vilivyopo maeneo hayo ni ya kusuasua, lakini kata nyingine mwitiko wake ni mkubwa.


Dk Mollel aliwataka wananchi kupuuza maneno ya mitaani ambayo hayana ushahidi wa kisayansi, badala yake wawapeleke watoto kupata chanjo hiyo muhimu.


Alisema sambamba na chanjo za ugonjwa huo, pia kutakuwa na utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za kukinga magonjwa ya minyoo, matende na ngiri maji.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu alisema amekerwa na wanaosambaza uvumi huo, huku akiwataka wananchi kupuuzia taarifa hizo za mitaani.


“Hakuna Serikali yoyote duniani inayoweza kutoa dawa kwa ajili ya kuathiri watu wake,”alisema.


Alisema dawa hizo ni sahihi na salama zenye lengo la kulinda afya za watoto na hazina madhara kwa binadamu.


Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donald Mbando alikaririwa akisema kuwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatarajia kufikia watoto zaidi ya 21 milioni wenye umri kuanzia miezi tisa hadi miaka 15.


Lengo la kampeni shirikishi ya ugonjwa wa surua na rubella ni kuhakikisha magonjwa yanayoepukika kwa chanjo yananatokomezwa.