Monday, October 20, 2014

SARE ZA JESHI ZAMPONZA DIAMOND PLATNUMZ, KUFIKISHWA MAHAKAMANI

MSANII nyota wa muziki wa Bongo Flava nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ huenda akaingia matatani baada ya juzi kupanda jukwaani kutumbuiza katika Tamasha la Serengeti Fiesta 2014 akiwa amevaa sare ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kinyume cha sheria.
Tangu msanii huyo afanye hivyo, mjadala umeibuka kwa wengi wao kujiuliza nini maana yake na kama alifanya hivyo kwa kibali maalumu au la, hasa ikizingatiwa ni hivi karibuni Jeshi hilo lilitoa onyo kwa wasanii na wengineo kutotumia mavazi hayo.
Mbali ya Diamond, hata vijana wake nao walishambulia jukwaa wakiwa katika mavazi hayo, akiwemo msanii aliyemshirikisha katika moja ya nyimbo zake, Ney wa Mitego.

Wakati shoo hiyo ikiendelea, baadhi ya mashabiki walianza kumzomea kila alipoimba kabla ya video kubwa ambazo zilikuwa mbele ya jukwaa hilo kuanza kuonyesha picha za mnato na video za mwanamuziki huyo akiwa amevaa mavazi hayo huku akiwa kama askari ‘anayekoki’ risasi katika katika bastora na baadaye katika bunduki ya kivita.
Kitendo hicho, kilionekama kuwakera zaidi maelfu ya wapenzi na mashabiki wa muziki waliokuwa wamejazana katika viwanja vya Leaders Club, huku kila mmoja akiwa na tafsiri yake.
Baada ya tukio hilo la juzi usiku, kitendo cha nyota huyo kuvalia mavazi hayo ya JWTZ, kimeibua mjadala hadi katika mitandao ya kijamii kuanzia jana asubuhi, ambapo picha za msanii huyo zikitumika kujenga hoja ya uhalali wa kufanya hivyo, huku vijana kadhaa wanaokutwa nazo mitaani wakiteswa vibaya na jeshi hilo.
Kwa upande wake Diamond, alitoa taarifa ndefu katika ukurasa wake wa Facebook na Instagram, akiishia kuelezea ni kwa nini alizomewa katika shoo hiyo.
Tanzania Daima ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura juu ya kitendo cha msanii huyo, alisema alikuwa hajui chochote na kuahidi kulifanyia kazi kama atapelekewa taarifa na wasaidizi wake.
Alipotafutwa Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Msanja, simu yake iliita bila kupokelewa na alipotafutwa msaidizi wake, alikiri kupata taarifa na kujionea kupitia shoo hiyo, huku akisisitiza bosi wake anaweza kulizungumzia hilo.
Tukio hilo limefanyika ikiwa ni siku chache tu tangu kijana mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya kijeshi maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kuvuliwa na kupewa adhabu ya kuogelea katika dimbwi la maji machafu yaliyotuama.
Aidha, msanii Gwamaka Kaihula ‘Crazy GK’ aliwahi kuhojiwa na Jeshi hilo kwa kutumia mavazi ya kijeshi katika kibao chake cha Simba wa Afrika, ambapo alijitetea pamoja na kuomba msamaha kwa kilichofanyika.
Kutokana na wimbi la watu mbalimbali hasa wasanii kuvalia mavazi yanayofanana na sare za jeshi hilo, hivi karibuni Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ, ilionya kama ifuatavyo:
Kumejitokeza kama fasheni kwa baadhi ya wasanii, hasa wanamuziki wa Bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare za jeshi kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.
Inawezekana kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo hawafahamu ni kinyume cha sheria ya nchi kukutwa nazo, ingawa kutokujua sheria bado sio utetezi mbele ya mahakama.
Mtu yeyote yule asiye na ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare za jeshi, atakuwa ametenda kosa, kwa hiyo atafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Katika uvaaji au uingizaji nguo, kama itatokea kwamba nguo hizo zinafanana kwa aina yoyote ile na zile za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ikadhaniwa kuwa ni hizo, mtu huyo ana hatia na anastahili kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi zilizopo
ilifafanua taarifa hiyo.