Wednesday, October 15, 2014

SIMULIZI; NAMNA FREEMASON ILIVYOINGIA TANZANIA , AFRIKA MASHARIKI ...SOMA ZAIDI

Wakati ule, hata hivyo, Ofisi ya Freemason Afrika Mashariki ilikuwa imetoa mchango mkubwa katika kusaidia kuimarisha ufreemason katika sehemu za bara.
Hatua ya kwanza ya Freemason ilikuwa ni kuimarisha uchumi, biashara na shughuli za kisiasa. Baadaye nguvu ikaelekezwa zaidi eneo la bara la Afrika Mashariki, siyo kwa Wajerumani wa Afrika Mashariki, bali kwa Wakenya, ambapo kukamilika kwa ujenzi wa reli ya Uganda kulikuwa tayari kumeanza kuonyesha matokeo mazuri katika eneo kubwa lililokuwa makazi ya wazungu Afrika Mashariki.
Zanzibar ilikuwa tayari imeshapiga hatua nzuri katika masuala la kilimo, biashara na miundombinu wakati huo.
Mwaka 1901, bidhaa ya kwanza ya majani ya chai Afrika Mashariki ilitengenezwa huko Dunga.  Mwanzoni majani hayo yalilimwa kwenye bustani iliyoanzishwa mwaka 1899.  Majani yalikuwa yakitengenezwa kwa kutumua zana za mikono, kuanikwa juani na kukaangwa kwa kutumia jiko la kawaida la mkaa.
Baadaye mwaka uleule, kiwanda cha kwanza cha mafuta kilianzishwa Zanzibar kikifuatiwa na ujenzi wa tangi katika mji wa Mtakuja. Tangi hilo lililowekwa na Messrs Smith Mackenzie na kampuni yake kama wakala wa Kampuni ya usafirishaji na biashara ya Shell Ltd, lilikuwa kwa ajili ya kukusanya mafuta mengi.
Pia kampuni hiyo ilijenga kiwanda kwa ajili ya kutengeneza mapipa ya kuwekea mafuta ya taa.
Mwaka 1903, gazeti la kwanza huko Zanzibar lililojulikana kama “Samachar” lilichapishwa. Baadaye gazeti hilo lilikuwa likichapishwa kila siku, huku chapisho lake la kwanza likitoka Agosti 21, 1905. Baadaye magazeti mengi tu yalichapishwa Zanzibar.
Mwaka 1903, nyumba nzuri zilijengwa Kigomasha huko Pemba na Chumbe. Mwaka uliofuata, Freemason Kenya waliomba kupewa hati ya kutambuliwa ili waanzishe ofisi.
Ofisi hiyo Namba 3084 ilifunguliwa rasmi Mei mosi, 1905. Baadaye, ilipandishwa ngazi ya juu zaidi. Mimi ni mwanachama katika ngazi hiyo.
Sultani wa Zanzibar alisisitiza ujenzi wa miundombinu. Ufaransa walifungua ofisi ya posta iliyokuwa ikitoa stempu za aina mbalimbali baada ya kuwepo zilizotolewa na nchi hiyo kati ya mwaka 1870 na 1900.
Shule ya familia ya kifalme na Waarabu daraja la pili ilifunguliwa, huku kampuni ya Marekani ikijenga njia ya reli kuunganisha Bububu na Forodhani na baadaye kuiuzia Serikali mwaka 1911.
Mwaka 1905, nyaya za umeme zilifungwa umbali wa maili tano kuzunguka kasri la mfalme. Kazi hiyo ilifanywa na Mr J.A. Jones wa New YORK
Kitu cha kuvutia, mitaa ya Zanzibar ilikuwa na umeme mapema zaidi kuliko mitaa ya London, ambako walikuwa bado wanatumia taa za gesi.
Kampuni ya Marekani ilifunga huduma ya simu katika kituo cha simu cha Old Fort na Ofisi ya Posta huko Shangani.
Hata hivyo, huduma za posta ambazo zilikuwa zimeanza mwaka 1873 katika jengo la Mackenzie zilikuwa tayari zimeunganishwa na umoja wa posta.
Reli  ya Uganda ilikuwa imeanzisha njia ya kuimarisha ukoloni zaidi katika eneo la bara. Jambo hili lilileta maendeleo na kuanzishwa kwa makazi mapya Kenya na Uganda.
Kadri ya muda ulivyokwenda, baadaye maeneo hayo yalikuja kuwa vituo muhimu vya Freemason kukua na kupanuka katika eneo lote la Afrika Mashariki.
Ofisi ya Freemason namba 3084 ilifanya kazi nzuri sana. Kazi ya kwanza ya Freemason mjini Nairobi ilikuwa kuhakikisha idadi ya wanachama inaongezeka.
Katika kufanikisha jambo hilo, ofisi iliamua kuwapandisha ngazi wanachama wote katika mkutano mmoja jambo ambalo linazuiwa na katiba ya Freemason.
Ofisi iliweka makazi yake ndani ya jengo la Posta katika mtaa wa Victoria (siku hizi unaitwa Tom Mboya). Ilikuwa ikitumia kinanda ilichoazima kutoka Kanisa la Mtakatifu Stefano. Ofisi hiyo ikiwa chini ya mwangalizi kutoka Scotland, ambaye ofisi yake iliitwa Scotia namba 1008, ilianzishwa mwaka 1906.
Kijana mdogo mwanachama katika ofisi ya Harmony aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa ofisi ya Scotia. Kutokana na ofisi ya Harmony kuisaidia ofisi ya kwanza ya Scotland wakati wa kufanya sherehe zao, utamaduni na mambo mengine, utaratibu huo ulizoeleka kwenye mfumo mzima kiasi cha kuleta utata kwa wanachama wa Freemason kati ya ofisi hizo mbili.
Kwa miaka mingine sita, Sir Charles Bowring, ambaye alitumika kama gavana wa makazi awamu  tatu, alitoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Freemason Kenya na Uganda.  Alikuja kuteuliwa kuwa Mkuu wa kwanza wa uchaguzi kwa nchi za Afrika Mashariki.
Miaka miwili baadaye, mwaka 1909 na 1910, yalitokea mambo makubwa mawili ambayo yalionyesha ukuaji wa Freemason Afrika Mashariki. Septemba 1909, ofisi ya Harmon namba 3084 ilipewa heshima ya kutembelewa na Rais wa Marekani, Theodore Roosevelt – mwanachama wa Freemason aliyekuwa amemaliza kwa mafanikio katika muda wake wa mihula miwili kama Rais ndani ya Ikulu ya Marekani.
Roosevelt alikuwa amekuja Afrika kwa mwaliko wa Taasisi ya Smithsonian ya Washington. Ziara yake ilisherehekewa zaidi kwa kumtunuku tuzo nyingi kuliko alivyotarajia kutoka kwenye taasisi ya kitaaluma.
Roosevelt aliteuliwa mwanachama wa heshima wa ofisi ya Freemason. Picha na sahihi yake bado vipo kwenye ofisi ya Nairobi.
Mfalme Arthur wa Connaught na Strathearn, alipoitembelea ofisi mwaka uliofuatia, alikuwa kiongozi mkuu wa ofisi ya Uingereza. Aliteuliwa Gavana mkuu wa ofisi ya Canada wakati alipopigiwa simu na ofisi ya Harmony.
Sarafu ya Rupia ya Waingereza wa Kihindi na fedha za noti zilianzishwa Zanzibar wakati huu. Gari la kwanza la Kijerumani la Daimler lilitumiwa na Sultani.
Magari aina ya Morris Cowley, Citreon na Fiat yaliingia Zanzibar na bara kipindi hicho. 
Mwaka 1911, mwaka ambao Sultani wa Zanzibar alihudhuria sherehe ya kumsimika Mfalme George V, ndiyo wakati ambapo ofisi ya Freemason tawi la Victoria Nyanza namba 3492 ilifunguliwa. Ilikuwa ya kwanza kufunguliwa Uganda.
Miaka miwili baadaye, ofisi ya Menengai namba 3559 na Mombasa namba 3645 zilifunguliwa. Mwanzoni mwa Vita ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914, jumla ya ofisi saba zilikuwa zimeshafunguliwa chini ya Katiba ya Kiingereza huku idadi ya wanachama ikikaribia mamia.
Vita ya dunia ilikwamisha maendeleo ya Freemason baada ya vijana wadogo wa Kiingereza kuingizwa jeshini. Pingamizi liliwekwa na vijana huko Zanzibar mwaka 1918. Ofisi ya pili ya Freemason ilifunguliwa Novemba 15 mwaka ule. 
Matokeo ya vita hayakuruhusu ofisi ya Zanzibar namba 3897 kusimikwa rasmi hadi Machi 29, 1920.
Gari la kwanza la mizigo tani mbili lilinunuliwa wakati ule, ambalo lilikuwa chini ya Idara ya kazi ya jamii.
Idara ya Kimataifa ya masuala ya bahari ilifanya kazi kati ya mwaka 1892 hadi 1920. Kituo cha kwanza cha kizani kilizinduliwa mwaka 1923 huku Serikali na Bunge la kwanza likirasimishwa mwaka 1926.
Kuondoka kwa utawala wa Kijerumani bara, kulichochea uanzishwaji wa ofisi za Freemason. Ofisi ya kwanza ya Freemason ilianzishwa Tabora na baadaye kuhamishiwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuwasaidia askari wa Kiingereza.