Sunday, October 12, 2014

TAIFA STARS YAREJESHA ENZI ZA RAHA, YAIFUMUA BENIN 4-1 TAIFA

TANZANIA imepata ushindi mnono dhidi ya Benin, wa mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hakizimana Louis, aliyesaidiwa na Simba Honore na Niyitegeta Jean Bosco wote wa Rwanda, hadi mapumziko, Stars tayari ilikuwa inaongoza mabao 2-0.
Mabao hayo yalifungwa na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16 na kiungo Amri Kiemba dakika ya 39.
Cannavaro alifunga bao hilo kwa kichwa baada ya kuruka katikati ya msitu wa mabeki wa Benin kuunganisha kona ya Erasto Edward Nyoni kutoka kulia.
Juma Luizio (katikati) akipongezwa baada ya kufunga bao la nne

Kiemba alifunga bao zuri mno akipokea pasi ya Mwinyi Kazimoto na kuanza ‘kuwapunguza’ mabeki wa Benin kabla ya kumchambua kipa wa Benin Farnoue Fabien.
Nyota wa West Bromwich Albion, Sessegnon Stephanne alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Stars, lakini hata hivyo walifanikiwa kumdhibiti asisababishe madhara.
Kipindi cha pili, Benin walianza na mabadiliko wakimpumzisha kipa wao wa kwanza mwenye umbo kubwa, Farnoue Fabien na kumuingiza Allagbe Saturnin.
Hata hivyo, kipa huyo alitunguliwa sawa na mwenzake, mabao mawili ndani ya dakika 45, huku Benin ikifanikiwa kupata bao la kufutia machozi.
Nadir Haroub 'Cannavaro' baada ya kufunga bao la kwanza
Amri Kiemba kushoto baada ya kufunga bao la pili
Kikosi cha Stars kilichoanza leo
Thomas Ulimwengu akimtoka beki wa Benin

Mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu aliifungia Stars bao la tatu dakika ya 49 akimalizia krosi fupi ya Mrisho Ngassa aliyemtoka vizuri beki wa Benin.
Mshambuliaji wa ZESCO United ya Zambia, Juma Luizio aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Ngassa, aliifungia Stars bao la nne akimalizia kazi nzuri ya Ulimwengu aliyemtoka beki wa Benin.
Benin ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Suanon Fadel dakika ya 90.
Stars, leo ikitumia mfumo wa 3-4-3 ilicheza vizuri na kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa na ingeweza kupata ushindi mnono zaidi- kama ingetumia vyema nafasi nyingine ilizotengeza.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Said Mourad dk75, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Oscar Joshua, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Salum Abubakar ‘Sure Boy’dk58, Haroun Chanongo/Said Ndemla dk77, Mrisho Ngassa/Juma Luizio dk60 na Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk86.
Benin; Farnoue Fabien/ Allagbe Saturnin dk46, Tossavi Eric, Ore Fortune/Dalmeida Sessy, Badarou Nana, Ogouchi Jean, Adeoti Jordan, Mama Seibom, Sessegnon Stephanne, Pote Mickael, Djigla David/Suanon Fadel dk49 na Dossou Jodel/Adudou Mohammed dk53.