Thursday, November 13, 2014

BARUA KWENU:MASTAA WA KIKE BONGO MOVIES MTAIGIZA MAISHA YENU HADI LINI?



Mastaa wa Bongo Movies. Bila shaka mko poa na mnaendelea na harakati zenu za kila siku, najua mna mishemishe nyingi kweli japo najua nyingi ni za starehe zaidi.Binafsi mimi niko poa naendelea na majukumu yangu ya kila siku ikiwemo hili la kuwaandikia barua. Madhumuni ya barua hii ni kama inavyojieleza hapo juu katika kichwa chake cha habari.
Ndugu zangu, nimekuwa nikifuatilia aina ya maisha mnayoishi kwa muda mrefu nimegundua wengi wenu mnaishi maisha ya kuigiza kama vile mnavyofanya kwenye filamu zenu. Hamtegemei kazi zenu kuendesha maisha bali mnatumia ‘njia’ mbadala ili kulinda heshima ya umaarufu wenu, siyo sawa.
Mnataka kuonekana mnakula katika mahoteli ya gharama, nyumba za gharama, kubadili mavazi kila siku, kuendesha magari ya kifahari na kila aina ya starehe mjini ili muweze kwenda sawa na wenye nazo.Ufahari mnaouonesha haufanani kabisa na pato mnaloingiza kwenye filamu (mifano ipo mingi tu).
Natambua kabisa bei ya sinema moja mnavyoiuza kwa wahindi au kwingineko, haitoshi kabisa kufanya vurugu ambazo mnazifanya kila siku wakati wengi wenu hata hamzalishi hata muvi tatu kwa mwaka.Dada zangu nataka tu niwakumbushe kwamba maisha si starehe tu, maisha yana maana kubwa kama mtajiheshimu na kutengeneza mazingira mazuri ya kutegemea kipato cha sanaa yenu, kuiboresha kwa kuwekeza nguvu na akili nyingi.

Sitaki kuwataja kwa majina kwa leo lakini naamini mnajijua. Kwa nini msifanye kazi kama baadhi ya mastaa wa kiume ambao tunawaona wanaingiza fedha na kuendesha maisha yao kupitia filamu wanazozizalisha? Kwa nini msiige mifano kutoka kwa dada zetu wa Nigeria ambao wanategemea sanaa kutengeneza mamilioni?
Badala msimame katika mfumo mzuri wa kuzalisha sinema kwa nguvu na akili zenu zote, nyinyi mnatumia njia ya mkato kujiingizia fedha. Madhara yake ndiyo mnajikuta mkiingia katika mtego wa kujiuza kama ilivyotokea kwa Jack Pentezel ‘Jack wa Chuz’, Aunty Lulu na Baby Madaha.
Ni rahisi mtu kuwarubuni kwa fedha, kuwanunulia magari ya kifahari na nyinyi mkaridhika na kuona mmeyapatia maisha. Kesho na kesho kutwa ndiyo haohao wanaokuja kuwanyang’anya baada ya kuwatumia vya kutosha sababu wanakuwa hawajawakabidhi kadi.
Ni aibu hata kwa mashabiki wenu ambao wanawafuatilia kupitia filamu. Wanavyoona mnaigiza maisha katika mitandao ya kijamii wanapata hamasa kwamba sanaa inawalipa kumbe kiuhalisia haiwalipi.Jamani badilikeni kwa kujituma katika kuigiza ili heshima ya majina yenu itokane na sanaa.
Naamini inawezekana kwani vipaji mnavyo na hakuna ubishi mnaweza kuibadilisha tasnia kama wenyewe mtaamua kufanya hivyo. Kwa leo acha niishie hapo, badilikeni!