Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limemtia mbaroni mganga mmoja wa jadi anayedaiwa kuteka watoto kwa njia za kishirikina kwa ajili ya kutolewa kafara.
Mbali na mganga huyo, pia wamemtia mbaroni mwanamke mmoja, anayedaiwa kusuka mipango ya kutekwa nyara kwa watoto na kuwahifadhi kwa mganga huyo.
Mganga huyo ambaye anadaiwa ni mwenyeji wa mkoani Mbeya, alikutwa na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13, akiwa tayari amepumbazwa tayari kumpeleka Mbozi mkoani Mbeya. Mtoto huyo aliyemaliza darasa la saba mapema mwaka huu Shule ya Msingi Majengo katika Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa waliofaulu katika mtihani wa Taifa.
Kwa mujibu wa habari hizo, mganga huyo (jina tunalo), anadaiwa kushirikiana na mwanamke mmoja, mkazi wa TPC kula njama za kumteka mtoto huyo. “Huyo mwanamke ndiye alishirikiana na huyo mganga kumteka mtoto kwa lengo la kumpeleka Mbozi, mkoani Mbeya na ajabu ni kwamba naye alikuwa akishiriki kumtafuta,” imedokezwa.
Kulingana na chanzo hicho, kiini cha kugundulika kwa mpango huo ni baada ya mwanamke huyo kwenda na rafiki yake kwa mganga, ikiwa ni maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kusafiri.
“Walipeleka chakula kwa huyo mganga na walipoingia ndani ndipo rafiki yake akamuuliza mbona huyu mtoto, ndiye anayetafutwa,” alidokeza mmoja wa ndugu wa mtoto na kuongeza:
“Huyo mwanamke ndiyo akamwambia naomba unyamaze kwa sababu huyu mtoto anasafiri kwenda Mbozi na mganga na wazazi wake hawatakaa wamwone tena na ndiyo maana nimeleta na hili begi.”
Hata hivyo, rafiki huyo aliamua kuvujisha siri hiyo kwa ndugu wa mtoto huyo kuwa amefichwa nyumbani kwa mganga huyo na ndipo ndugu walipomfuata kwa mganga.
Akizungumza na gazeti hili nje ya kituo cha kati cha polisi mjini Moshi, Prosper Swai ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo, alisema mwanaye alitoweka Novemba 2 na baada ya kutoonekana alitoa taarifa kituo cha Polisi cha TPC na kwa uongozi wa kijiji na juhudi za kumtafuta hazikuzaa matunda.
Swai alisema baada ya siku tano, alipata taarifa kwa mtu mmoja kuwa mwanae amehifadhiwa nyumbani kwa mganga na alipelekwa na mwanamke huyo.
Baada ya kupata taarifa hizo, akiwa na polisi na uongozi wa kijiji, walivamia nyumba ya mganga huyo na kumkuta mtoto akiwa amelala chini kwenye mfuko wa mbolea akiwa hajitambui.
Alifafanua kuwa baada ya kumpata mtoto huyo, alimkagua na kumkuta na hirizi kubwa kiunoni hali iliyomfanya aogope kuwa mwanae huyo aliibwa kwa lengo la kutolewa kafara.
Swai alisema matukio ya wizi wa watoto katika eneo la TPC na maeneo ya jirani yamekithiri na katika kipindi cha mwezi mmoja, watoto wanne wamepotea katika mazingira hayo.
Alisema wawili kati yao ni wakazi wa Kijiji cha Langasani na walikutwa wamekatwa viungo na kutupwa msituni wakati mtoto mwingine ni wa Kijiji cha Chekereni ambaye bado hajapatikana.
Mtoto mwingine ni wa Kijiji cha Mbugani alitoweka juzi baada ya baba yake kumtuma kwenda kukagua tanuru la matofali na hadi jana mchana alikuwa hajapatikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alikiri kumshikilia mganga huyo na watu wengine wanaodaiwa kuhusika kumpeleka mtoto huyo kwa mganga huyo na kuwa atatoa taarifa baada ya kukusanya taarifa zaidi.