Friday, December 26, 2014

HUKU MKEWE AKISOTA GEREZANI MISS TZ AOLEWA NA MUME WA JACK PATRICK

DUNIA ina mambo! Wakati mkewe mwanamitindo Jacqueline Fitzpatrick Cliff ‘Jack Patrick’ akiwa nyuma ya nondo kwa msala wa madawa ya kulevya ‘unga’ nchini China, mumewe, Abdulatif Fundikira ‘Tif’ amefunga ndoa ya siri na Miss Tanzania 2011, Salha Israel, Amani linakupa mchapo kamili. 
 
Mume wa ‘Jack Patrick’, Abdulatif Fundikira ‘Tif’ akifunga ndoa ya siri na Miss Tanzania 2011, Salha Israel(liyeshika karatasi).
 TUJIUNGE NA CHANZO
 Kwa mujibu wa chanzo makini, uhusiano wa Salha na Tif uliibuka na kushamiri mwaka jana baada ya Jack kukamatwa na unga huo.“Penzi lao liliibuka ghafla tu, jamaa naona ana ‘aleji’ na warembo wenye majina yao maana penzi lake na Jack lilipoyumba na kisha mrembo huyo kukamatwa na madawa ya kulevya nchini China, fasta akaanzisha uhusiano na Salha,” kilisema chanzo hicho.
 UMAARUFU WA JACK UPOJE?
Jack ni mshiriki wa Miss Tanzania mwaka 2006 akitokea Miss Ilala lakini umaarufu wake ulizidi kukua baada ya kushiriki kama ‘video queen’ katika video mbalimbali za wasanii wa muziki wa Bongo Fleva ikiwemo video ya She Got Gwan ya marehemu Albert Mangwea.


Miss Tanzania 2011, Salha Israel akipozi.
 VYANZO VINGINE
Hata hivyo, vyanzo vingine vimeeleza kuwa, Jack na mumewe walikuwa na mgogoro mzito kabla modo huyo hajakamatwa na madawa ya kulevya.“Walikuwa na mgogoro, ilifika wakati Jack alikuwa akidai talaka mahakamani lakini bahati mbaya kabla hajafanikiwa kupewa akaswekwa nyuma ya ndondo,” kilieleza chanzo hicho.

 NDOA ILIVYOFUNGWA
Chanzo chetu kilichoshuhudia tukio hilo la siri kilieleza kuwa, Tif na Salha walifunga ndoa ya kiserikali Jumapili iliyopita Sinza-Mori jijini Dar, nyumbani kwa wazazi wa  Salha ambapo sherehe hiyo ilihudhuriwa na watu wachache ikisemekana ndugu wa pande zote mbili ndiyo walitawala zaidi.

 “Kwenye hiyo ndoa hakukuwa na watu wengi, sanasana ndugu tena ilifungwa kwa siri sana, hawakupenda watu wengi wajue  kuhusiana na shughuli hiyo, hata wapiga picha walizuiwa kabisa kupiga picha katika simu zao,” kilisema chanzo hicho.


Mwanamitindo, Jacqueline Fitzpatrick Cliff ‘Jack Patrick’.
 PICHA ZAPATIKANA
Katika kufukunyua uthibitisho wa taarifa hizo, mwanahabari wetu alifanikiwa kuzinasa picha za tukio hilo ambazo zinamuonesha Salha akiwa na Abdulatif pamoja na ndugu wachache wa pande zote mbili muda mfupi baada ya ndoa kufungwa.

 JACK ATONYWA
Wakati mwanahabari wetu akizidi kuichimba habari hiyo juzi, alikutana ndugu wa Jack ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini. Alikiri kusikia ndoa hiyo na kuweka wazi kuwa taarifa zimemfikia Jack na kumfanya apate presha.

 “Jack amepelekewa taarifa hizo Jumapili ileile, ameshtuka na presha ikampanda ingawa haikumchukua muda mrefu akarudi katika hali yake ya kawaida maana si unajua Jack na Salha ni marafiki!” alisema ndugu huyo.

‘Jack Patrick’ wakati akifunga ndoa na mumewe Abdulatif Fundikira ‘Tif’.
 SALHA ANASEMAJE?
Amani lilimtafuta Salha kwa njia ya simu ili kujua anazungumziaje ndoa yake hiyo na Tof lakini simu yake haikuwa hewani muda mrefu.
Amani linaendelea kumtafuta, akipatikana atafunguka kwa kirefu zaidi.

 TUJIKUMBUSHE
Tif na Jack walifunga ndoa Desemba 3, 2011 katika ufukwe wa Hoteli ya Coral, Masaki jijini Dar es Salaam. Ndoa hiyo ilifungwa na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Hatibu Benard.

 Mwaka mmoja baadaye, ndoa hiyo iliingia mdudu ambapo mzozo kwa wawili huo uliibuka kiasi cha kufikia hata Jack kushindwa kufika Gereza la Keko, Dar pale Tif alipotupwa mahabusu kwa madai ya kujihusisha na madawa ya kulevya. Mwishowe wawili hao walimwagana na Jack kupata msala na yeye wa kukutwa na madawa ya kulevya nchini China, Desemba mwaka jana ambako alihukumiwa kifungo cha miaka 7 jela.