Thursday, December 11, 2014

MAMILIONI YA IDRIS YAZUA VITA KATI YA WATANZANIA NA WANIGERIA

MILIONI 510 alizonyakua mshindi wa Shindano la Big Brother Hotshot (2014), Idris Sultan ndiyo habari ya mjini. Tayari fedha hizo zimezua vita nzito kati ya Wanijeria na Wabongo, Risasi Mchanganyiko linakupa sakata zima hatua kwa hatua.
Idris Sultan akirurahia baada ya kutangazwa mshindi wa Shindano la Big Brother Hotshot (2014).
Ushindi huo wa kishindo alioupata Idris, ulifanyika usiku wa Jumapili iliyopita pande za Johanesburgy, Afrika Kusini ambapo mshindi huyo kutoka Tanzania aliwagalagaza washiriki wenzake kutoka mataifa ya Zimbabwe (Butterphly), Ghana (M’am Bea), Zambia (Macky2), Afrika Kusini (Nhlanhla), Malawi (Sipe) na Naigeria (Tayo).
USIKU WA TUKIO
Tofauti na miaka mingine ambayo shindano hilo lilikuwa likikosa msisimko katika mitandao ya kijamii, siku hiyo watu wengi walikuwa kwenye runinga zao wakifuatilia huku wengine wakitumia mitandao ya kijamii kupashana habari.
KURA ZA KUMWAGA
Siku chache kuelekea kwenye kilele cha mashindano hayo, ilifanyika jitihada kubwa kutoka kwa wasanii, wadau na watu wa kawaida kuhamasisha jamii iendelee kumpigia kura ili aweze kuibuka kidedea na kuliletea taifa heshima.
Akipongezwa na wenzie baada ya kutangazwa mshindiwa shindano hilo.
MAMBO YAJIPA
Kama ilivyokuwa maombi ya Wabongo wengi usiku huo, kweli ilipofika wakati wa kutangazwa mshindi, mtangazaji maarufu Mnaijeria, IK hakutangaza jina lingine zaidi ya Idris ambaye alikuwa na baraka zote kuanzia kwenye upigaji kura hadi ndani ya mjengo alikoishi kwa siku 63.
SHAMRASHARA ZA USHINDI
Ndani ya sekunde kadhaa tangu atangazwe, mitandao ya kijamii ililipuka kwa shangwe. Wasanii kama Joseph Haule ‘Prof Jay’, Nasibu Abdu ‘Diamond’, Elizabert Michael ‘Lulu’, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ na wengine wengi walitupia komenti kibao mitandaoni kuonesha kuguswa na ushindi huo.
DAVIDO ATIBUA SHUGHULI
Wakati kila mmoja akiendelea kushangilia ushindi huo mtandaoni, msanii ambaye alipata jina kubwa baada ya kuja Bongo mwaka jana katika shoo ya Serengeti Fiesta, David Adedeji Adeleke ‘Davido’ alitibua hali ya hewa baada ya kuweka maneno yaliyotafsiriwa kuwa ni kejeli kwa Wabongo.
Maneno hayo yalisomeka hivi: N they cheat again lol ( Na wamedanganya tena).
Idris Sultan akiwashukuru wote waliomuwezesha kushinda.
VITA YAIBUKA
Vita nzito iliibuka hapo na Wabongo wengi kuonekana kukasirishwa na kauli hiyo ambayo waliita ni ya kibaguzi ambayo ilikuwa na mlengo wa kuona tumeshinda kwa njia ya udanganyifu kwa mara nyingine.
Kila mmoja aliitafsiri kivyake, kuna ambao walimtukana Davido wakiamini amesema Wabongo wamedanganya kwa mara ya pili kwa maana ya kwanza ni ushindi wa Idris Big Brother na ya pili ni ya The Future Awards Africa (aliyoipata Diamond nchini Nigeria usiku huohuo).
Tafsiri ya kauli ya Davido ilizidi kuibua utata zaidi ambapo wengine ‘walimpaka’ nyota huyo wa Naigeria wakiamini tuzo za kwanza alizomaanisha ni zile za Channel O (Choamva) alizoshinda Daimond hivi karibuni na ya pili ni ya The Future Awards Nigeria.
Davido.
CHOKA AHAMASISHA DAVIDO KUFUTWA
Wakati bifu hilo likizidi kufukuta mitandaoni, DJ maarufu Bongo, Choka alianzisha kampeni ya Wabongo wote kumfuta urafiki Davido katika mtandao wa Instagram kwani ameonesha ubaguzi wa hali ya juu.
“Oi washkaji mnaonaje tukaanzisha kampeni hii, unfollow Davido, unfollow Davido...” aliandika DJ Choka.
DIAMOND AMJIBU
Kuonesha uzalendo, Diamond hakukaa kimya. Akaamua kumjibu kwa kuandika: “Thanks God we have cheated another one on The Future Awards Lagos Nigeria...sameday...same night, thank you Allah!”
Kwa tafsiri isiyo rasmi, Diamond alikuwa akimjibu Davido kwa kusema ‘Asante Mungu, tumedanganya tuzo nyingine ya The Future Award, ambayo tumeshinda siku na usiku huu huu hapa Lagos Nigeria’. Idris na Diamond walipata ushindi wao siku moja katika nchi mbili tofauti.
Mfano wa pesa alizopata Idris Sultan.
Akizungumza na paparazi wetu, mdau mkubwa wa burudani ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kwa namna yoyote ile Davido hakupaswa kuandika kauli ile ambayo imejenga uadui kwa Wabongo na Wanaigeria.
“Amekosea, mtu mwenye akili zake hawezi kuandika vile wakati anajua Bongo ndiyo iliyomfanya ajulikane zaidi kimataifa, kabla hajaja Bongo, nani alimjua kimataifa? Anatakiwa kuomba radhi kama anataka hii vita isiendelee maana sidhani kama anaweza kuja kupiga shoo Bongo na watu wakamfurahia tena,” alisema mdau huyo.
TUJIKUMBUSHE
Historia ya mashindano hayo inaonesha, kabla ya Idris ambaye alitarajiwa kuingia nchini leo, mwaka 2011, mshiriki Richard Dyle Bezuidenhout ndiye pekee aliyewahi kushinda.