Aliyekuwa kocha mkuu wa Simba, Patrick Phiri.
Na Nicodemus JonasANATIA huruma! Ndivyo unaweza kumuongelea Patrick Phiri aliyeachishwa kibarua ndani ya mechi nane alizoiongoza Simba ligi, ambapo jana alifunguka bayana kuwa aliacha ofa nzuri kutoka kwa Shirikisho la Soka Namibia ambapo alikuwa aende kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa, lakini akaamua kuja Simba kutokana na heshima aliyowapa.
Phiri ambaye alitarajia kuondoka jana amefungishiwa virago kwa kile kilichosemwa kuwa ni kutokana na mwenendo mbovu wa timu ambapo amefungwa mechi moja tu kati ya nane dhidi ya Kagera Sugar wiki iliyopita.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Phiri alisema kuwa kabla ya Simba kumhitaji alikuwa na ofa nzuri nchini Namibia, lakini aliamua kuja Simba kutokana na kuifahamu vema hivyo isingekuwa kazi ngumu kwake pia na mapenzi makubwa aliyonayo kwani ameifundisha mara kadhaa.
“Nilikuwa na ofa kule Namibia tena nzuri, lakini niliamua kuwasikiliza Simba kwa kuwa kwanza ni timu yangu, nimekuwa nao kwa muda mrefu, pia nilijua ingekuwa kazi rahisi kwangu kwa kuwa si mazingira mageni kwangu.
“Siwezi kusema kuwa Simba ilikuwa imenishinda ila wenye maamuzi ni wao (viongozi) wanaojua wapi penye udhaifu katika timu yao. Nadhani hii ni mara yangu ya tatu kuja Simba kwa hiyo nilijua mambo yangekuwa rahisi kwangu kutokana na kuifahamu vema,” alisema Mzambia huyo ambaye alikuwa akikunja kitita cha milioni nane kwa mwezi.
Nafasi yake imechukuliwa na Mserbia, Goran Kopunovic ambaye kibarua chake cha kwanza kitakuwa kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi huku Visiwani Zanzibar.