Thursday, January 1, 2015

HAWA NDO VIONGOZI WENYE VITUKO DUNIANI

Wakati kila mtu akiamini kuwa marais au viongozi wa nchi ni watu makini na wastaarabu hasa katika kufanya mambo yanayoendana na maadili na tamaduni za nchi zao, viongozi hawa ni kinyume chake ambapo katika vipindi tofauti vya utawala wao wameacha historia ya vituko mbalimbali vinavyowaacha wanahistoria wengi midomo wazi kwa kutoendana kabisa na nyadhifa walizonazo. Songa nayo…
Lyndon B. Johnson
Alikuwa rais wa 36 wa Marekani, ndiye rais anayelaumiwa sana kwa kuchochea vita kati ya taifa lake na Vietnam. Licha ya tabia yake ya kupenda sana wanawake ambapo katika utawala wake amedaiwa kutembea na masekretari wengi, alitajwa kuwa na tabia ya kukojoa mbele ya kadamnasi na mtu yeyote aliyeonesha kupinga kitendo chake hicho alimfungulia zipu.

Andrew Jackson
Ni rais wa saba wa Marekani ambaye anatajwa kuwa na tabia ya ajabu ya kucheza mchezo wa kupigana risasi maarufu kama ‘duel’ ambapo mtu hukaa upande mmoja wa meza na mwenzake upande mwingine wakitazamana kisha huingiza risasi ndani ya bastola zilizokuwa mezani wa kwanza kumaliza humshuti mwenzake na kuwa mshindi bila kujali atapoteza maisha au la.

Kutokana na mchezo huo, rais huyo alishawahi kuharibiwa bega lake kisha kuishi na risasi moja kifuani kwake siku zote za maisha yake zilizobaki baada ya mtu mmoja aliyecheza naye mchezo huo kumuwahi na kumpiga kifuani.
Herbert Hoover
Wakati marais wengine wakipendelea kufuga wanyama kama paka na mbwa, Herbert Hoover aliwapa kazi wafanyakazi wa ikulu ya Marekani wa wakati wake kwa kulazimika kumtunza mamba ambaye alikuwa mnyama kipenzi cha rais huyo wa 31.

Mobutu  Sese Seko
Alikuwa ni Rais wa Zaire ambayo sasa ni DRC, anakumbukwa kwa kituko chake cha kutunga sheria ya kukataza televisheni za Zaire kutotaja jina la mtu yeyote kwenye TV bali jina lake pekee huku akienda mbali zaidi kwa kuagiza kurushwa kwa picha inayomuonesha akishuka kutoka mawinguni kabla ya kuanza kwa habari za jioni. Mbali na hayo aliwafunga mamia ya Wazaire kwa kosa la kuwa na majina ya kizungu.

Idd Amin 
Alikuwa mtawala wa kidikteta nchini Uganda kuanzia mwaka 1971 hadi 1979. Pamoja na tabia ya ukatili wa hali ya juu aliyodaiwa kuwa nayo, anatajwa pia kuwa na chuki kali pindi alipotoswa kimapenzi na wanawake kadhaa aliowataka.

Inadaiwa kuwa hata sababu ya yeye kuwafukuza wafanyabiashara wa asili ya Asia nchini mwake ni kukataliwa kuoa binti wa Kihindi na baba wa msichana huyo ambaye alikuwa  mfanyabiashara mkubwa nchini  humo.
Idd Amin alienda mbali zaidi baada ya kumhamishia bifu hilo hadi Malkia wa Uingereza, Queen Elizabeth  baada ya kumuandikia mara kadhaa barua za kimapenzi akitaka kumuoa ambapo hakujibiwa hata moja. Inasemekana kuwa akiwa na ndoto za kumpata malkia huyo alifikia hatua ya kujiita mfalme wa Scotland ndoto ambazo hakuzifikia mwisho wake kwani aling’olewa madarakani.
Kim Jong II 
Ni kiongozi wa Korea Kaskazini aliyechukuwa madaraka tangu mwaka 1998 baada ya baba yake kufariki. Moja ya vituko vyake ni kwamba aliwahi kudai kuwa yeye ndiye mgunduzi wa baga ‘humburger’.

Ukiacha hilo aliingia katika kashfa ya kuwateka madairekta waliosifika sana kutoka Korea Kusini akiwataka wairudie filamu ya Godzillah iliyotengenezwa Marekani. Kim alienda mbali zaidi baada ya kutangaza kuwatokomeza wakazi wa mji wa Pyongyang kwa kosa la kuwa na watu wafupi wa kimo. Hii ilitokana na yeye mwenyewe kutokea kwenye jimbo hilo na kuwa mfupi kiasi cha kuchukia umbo lake.