Thursday, January 1, 2015

SIMBA YAPIGWA NA MTIBWA SUGAR KOMBE LA MAPINDUZI HUKO ZANZIBAR

MTIBWA Sugar imeanza vizuri michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuichapa Simba SC bao 1-0 katika mchezo wa Kundi C uliomalizika hivi karibuni Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mtibwa Sugar ilipata bao hilo kupitia kwa kiungo na Nahodha wa zamani wa Simba SC, Henry Joseph Shindika dakika ya 44 baada ya mabeki wa Simba SC kuzembea kuokoa mpira kwenye eneo la hatari kufuatia kona ya David Luhende.
Ikiongozwa na Kocha Msaidizi, Suleiman Matola baada ya kufukuzwa kwa kocha Mkuu, Mzambia, Patrick Phiri, Simba SC ilishindwa kufurukuta mbele ya Mtibwa, inayofundishwa na Mecky Mexime. 
Henry Joseph leo ameifunga timu yake ya zamani Simba SC

Kocha Mserbia, Goran Kopunovic aliyesaini Mkataba wa mwaka mmoja kurithi mikoba ya Phiri, alikuwepo jukwaani kushuhudia Simba SC ikicheza ovyo.
Wazi Simba SC ilionekana kuathiriwa na kuwakosa wachezaji wake Waganda, mabeki Juuko Murushid, Joseph Owino na washambuliaji Emmanuel Okwi na Simon Sserunkuma ambao bado wapo kwao, Kampala.
Mfungaji bora wa Ligi ya Kenya misimu miwili iliyopita, Dan Sserunkuma aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Gor Mahia ya Nairobi, aliingia kipindi cha pili, lakini hakupelekwa ya kutosha mipira licha ya kujipanga vizuri wakati wote timu ikishambulia.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Abdulaziz Makame/Jonas Mkude dk46, Awadh Juma, Elias Maguri, Said Ndemla/Shaaban Kisiga dk82, Ibrahim Hajibu/Dan Sserunkuma dk55, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Abdul Banda.
Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Said Mkopi, David Luhende, Ally Lundenga, Salim Mbonde, Henry Joseph, Ally Shomary, Muzamil Yassin, Ame Ally/Mussa Mgosi dk80, Ibrahim Jeba na Jamal Mnyate/Vincent Barnabas dk61.
Katika mechi za awali leo, JKU iliifunga mabao 2-0 Mafunzo mchezo wa Kundi C, mabao ya washindi yakifungwa na Amour Mohammed dakika ya saba na Isihaka Othman dakika ya 27.
Nayo Polisi imeifunga 1-0 Shaba katika mchezo wa Kundi A, bao pekee la Ali Khalid dakika ya 36.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi tatu pia, ya kwanza KMKM na Mtende, ya pili KCCA na Azam FC nay a mwisho Taifa jang’ombe Uwanja huo huo wa Amaan.