MADIWANI wa Halmashauri ya Nsimbo wilayani Mlele katika mkoa wa Katavi wameshauriwa kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kabla ya kuchukua fomu za kugombea nafasi ya udiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Diwani wa kata ya Kapalala, Reward Sichone alitoa ushauri huo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi, Diwani wa kata ya Sitalike, Silvester Nswima kuwasilisha taarifa kuhusu hali ya Ukimwi.
Hata hivyo Nswima alipinga ushauri huo wa Sichone, akisema suala la madiwani kupimwa afya zao kwa pamoja haiwezekani, kwani kupima ni hiyari ya kila mtu na si lazima, hivyo kila mtu atapima kwa muda wake na kwa hiyari yake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo, Mohammed Assenga alisema kitendo cha madiwani kupima afya zao kinaweza kuwa ni mfano mzuri kwa watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Nsimbo.