Tuesday, February 3, 2015

BAKHRESA ATUMIKA KUTAPELI...

MFANYABIASHARA tajiri Afrika Mashariki na Kati, Said Salum Bakhresa (pichani), jina lake limetumika katika utapeli jijini Dar baada ya watu waliodai ni wafanyakazi wake kumrubuni mkazi wa Kariakoo, Mussa Mohammed kuvunja fremu yenye duka lake ili kupisha ujenzi wa maegesho ya magari, Uwazi limedokezwa.
Mfanyabiashara tajiri Afrika Mashariki na Kati, Said Salum Bakhresa.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni katika  jijini Dar, Mohammed alisema wafanyakazi hao waliodai kutumwa na tajiri huyo, walimwambia baada ya kuvunja, duka jipya lingejengwa ndani ya siku kumi.
“Nilikataa kwani niliona siku kumi kukaa bila kufanya biashara ni nyingi na isitoshe yeye siyo mwenye duka nililopanga, hata hivyo, msimamizi wa mwenye nyumba walionipangisha, Juma alinisihi nikubali kwa vile wana nia nzuri, nilitoa vyombo nje, nikavifunika kwa turubai nikisuburi siku hiyo ya kujengewa.
“Siku kumi zilipita bila kunijengea duka, alikuja kwangu tena Huzefa akaniambia mzee Bakhresa amesema hapatajengwa tena kwani eneo ni lake, nilichanganyikiwa nikijiuliza fedha nilizokopa benki na kwa watu nitazirudishaje.
“Nilifunga safari mpaka kwa Bakhresa na kumwelezea, akanipa pole na kuniambia hapatajengwa  kwa madai eneo ni la kwake, akanishauri nishirikiane na Omari kutafuta  fremu nyingine ya biashara atalipia.
“Akaniambia tukishapata fremu malipo yatafanyika kupitia kwa Omari, kwa bahati nzuri tukapata sehemu Kariakoo ambapo kodi kwa mwezi ni milioni moja na nusu, walisema niandike kwa maandishi, nikafanya hivyo, ilikuwa ni kwa muda wa mwaka mmoja sawa na shilingi milioni kumi na nane.
“Nilimpa Omari akampelekea lakini mpaka sasa sijapata jibu na nikiomba nimuone Bakhresa hawataki, wananifukuza, nikimpigia Omari simu  hapokei, akipokea ananijibu vibaya ingawa yeye ndiye aliyeambiwa atamaliza kila kitu, nimekuwa kama adui.
Bw. Mussa Mohammed anyedai kurubuniwa na watu waliodai kuwa ni wafanyakazi waBakhresa.
“Siku moja nilikutana na Omari nilimuulizia akasema mzee amesema atanipa milioni moja tu na siyo kwa sasa, nilijisikia vibaya kwani nanyeshewa mvua hapa nje, familia yangu inateseka, watoto wangu hawasomi, nashindwa kurejesha mkopo, mali yangu inaharibika wao hawajali, nataka nimuone Bakhresa uso kwa uso maana inawezekana ameshatoa fedha ikaliwa na wajanja,” alisema Mohammed.
Msimamizi wa mwenye nyumba iliyokuwa na duka la Mohammed, Juma alikiri kwamba duka lililovunjwa lipo katika eneo lao na hata kodi walikuwa wanalipwa wao, akidai suala hilo ni la kibabe na ameahidi kumtafuta Bakhresa ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Omari alipotafutwa kwa njia ya simu alisema suala hilo analijua na mzee Bakhresa ndiye aliyemtuma alisimamie na kwamba kuhusu malipo mlalamikaji hatapata chochote kwa vile eneo lile ni la Bakhresa.
Hata hivyo, gazeti hili bado linahitaji kujiridhisha ili kujua kwa nini Bakhresa anatajwa mara kwa mara wakati kiuhalisia, baada ya duka hilo kuvunjwa kwa ushauri wa mmiliki wake, ambaye ndiye aliyekuwa akilipwa kodi ya pango na mlalamikaji, ndiye aliyepaswa kulalamikiwa na Mohammed.
Kwa mujibu wa Mohammed, alilipa kodi ya mwaka mmoja kwa mwenye nyumba huyo, ambaye hata hivyo, hasemi lolote juu ya madai ya wapambe wa Bakhresa wanaodai eneo hilo ni la mzee huyo tajiri. Uwazi linafuatilia kwa karibu sakata hili.