Thursday, February 12, 2015

HAYA NDIYO MAPYA YALIYOIBUKA KUHUSU TUKIO LA MME KUMCHINJA MKE WAKE




Na Makongoro Oging’/Uwazi
SIKU chache zimepita tangu Remy Joseph,
35, (pichani) kudaiwa kumuua kwa
kumchinja na kisu mkewe, Josephine Mushi
kwenye Hoteli ya Friends Corner iliyopo
Manzese jijini Dar, mengine yamebainika,
Uwazi limechimba zaidi.
Taarifa kutoka vyanzo vya habari hotelini
hapo zinadai kuwa, saa tano asubuhi ya
Januari 23, mwaka huu, mwanamume huyo
alifika kwenye hoteli hiyo na kufanya
sherehe ya kuzaliwa kwake ‘bethidei’
ambapo alikuwa akitimiza miaka 35.
Mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo
ambaye hakupenda jina lake liandikwe
gazetini alisema siku hiyo mtuhumiwa huyo
alifika akiwa na mwanamke mweupe (jina
halikupatikana) ambaye wahudumu wote
walijua ndiye mke wake kutokana na kuwa
mstari wa mbele katika shamrashamra
hiyo.“Sisi tulimuona ni kijana mstaarabu na
haya ya mauaji yasingetokea, lakini kumbe
alikuwa akisherehekea huku akijua atamuua
mkewe siku si nyingi mbele tena kwenye
hoteli hiihii, kwa kweli imetushangaza
sana,” alisema mhudumu huyo.
Uwazi lilimtafuta mkurugenzi wa hoteli hiyo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Massawe
ambapo alikiri kupata taarifa ya sherehe
hiyo kutoka kwa wahudumu wake lakini
hakujua alichodhamiria mtuhumiwa huyo
mpaka mauaji yalipofanyika na kubainika
kuwa, kumbe ni yeye aliyekuwa ameandaa
sherehe
Joseph alikutwa na polisi katika chumba
kimoja cha hoteli hiyo akiwa na kisu
mkononi muda mfupi baada ya kumchinja
mkewe wake na yeye kutaka kujiua lakini
akashindwa.
Ilidaiwa kuwa, Joseph alipanga hotelini hapo
Januari 28, mwaka huu huku akiwa na
mkewe huyo lakini siku ya pili wahudumu
waliona damu zikitiririka kutoka chumbani
kupitia mlangoni. Waliita polisi na
walipofika walibaini kufanyika kwa mauaji
hayo ya kinyama.
Mtuhumiwa bado yupo Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa matibabu chini ya ulinzi
mkali wa polisi huku mkewe akizikwa Moshi,
Februari Mosi mwaka huu