Sunday, February 1, 2015

"Kamishna wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja anaweza kuwa anashirikiana na Majambazi wanaoiba risasi vituo vya polisi"...Godbless Lema


MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), jana alimshambulia kwa maneno makali Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, kuwa anaweza kuwa anashirikiana na majambazi wanaovamia vituo vya polisi na kupora silaha.
 
Lema alitoa maneno hayo makali ya kumshambulia Chagonja bungeni jana, wakati akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
 
Akichangia hoja hizo, Lema aliliambia Bunge kuwa Chagonja anaweza kuwa anahusika katika matukio ya ujambazi katika vituo vya polisi kwa sababu anataka kudhoofisha utendaji kazi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
 
Katika maelezo yake hayo, Lema alilifananisha taifa na chumba kinachotumiwa na vijana wa kihuni kuishi ambacho hakina utaratibu unaoeleweka wa muda wa maakuli na malazi.
 
“Mheshimiwa Mwenyekiti, geto ni mahali ambapo watu wanaishi bila kufuata utaratibu, yaani katika geto, wakati wa kulala anayewahi ndiye anayelala kitandani.
 
"Geto chakula kinapopikwa kinaweza kuliwa hata kama hakijaiva, kwa hiyo nchi hii naifananisha na geto kwa sababu watu wanaiba fedha za umma kama wanavyotaka.
 
“Katika ripoti za Bunge zilizosomwa hapa jana (juzi) zimejaa wizi, kila ukurasa wa taarifa ya Zitto ni wizi tu, wizi tu, hivi huu wizi utakwisha lini? Hata zile bunduki zinazoibwa katika vituo vya polisi zinaweza kuwa ni ‘sabotage’ (hujuma), zinazofanywa na Chagonja dhidi ya IGP,”alisema Lema.
 

Alisema amefanya uchunguzi wake binafsi uliobaini kuwa Jeshi la Polisi limegawanyika na kwamba haamini kama Rais Jakaya Kikwete amekwishafanya mabadiliko ya uongozi ndani ya jeshi hilo.