Askari sita wakiwemo wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wamejeruhiwa vibaya kwa risasi wakati wa mapigano baina yao na watu wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu wakati wa Msako Maalum wa kutafuta silaha zinazodaiwa kufichwa kwenye moja ya eneo la mapango ya Amboni.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, amebainisha hayo alasiri ya jana, wakati akitoa taarifa kwa wanahabari jijini Tanga kuhusu hali ya matukio ya uhalifu yanayoendelea jijini humo.
Alisema mapambano hayo yalitokea muda mfupi tu wakati wa msako maalum wa kutafuta silaha zinazodaiwa kufichwa kwenye moja ya eneo la mapango ya Amboni, yaliyoko umbali wa kilometa 10 kutoka katikati ya Jiji la Tanga.
“Baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wasiri wetu ndipo alfajiri ya leo (jana) askari wetu walienda eneo la tukio kwa lengo la kutafuta hizo silaha na ghafla wakavamiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa wamejificha”, alisema.
Alisema kujeruhiwa kwao kumetokana na mapambano ya kurushiana risasi yaliyodumu kwa dakika 15 alfajiri ya kuamkia jana katika mashimo ya mawe ambayo yako jirani na mapango ya Amboni.
Kamishna Chagonja alisema chanzo cha mapambao hayo, ni tukio la Januari 26 mwaka huu, wakati askari wawili walipovamiwa na watu wasiojulikana na kunyang’anywa bunduki mbili aiana ya SMG, zilizokuwa na risasi 60.
“Upelelezi wetu uliendelea baada ya tukio hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kuwasaka na tukafanikiwa kupata wahalifu…jana asubuhi tuliarifiwa kwamba silaha hizo zimefichwa kwenye moja ya mapango ya Amboni na ndiko wakapeleka askari huko ili kuzitafuta,”alisema.
“Wakati askari hao wakiendelea kutafuta, ghafla walivamiwa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa wamejificha kwenye eneo lingine la pango hilo …ikalazimika wajibu mapigo,” alisema.
Kamishna Chagonja alisema baada ya kuzima mapigano, waliamua kuingia ndani ya mapango hayo na kukuta vifaa mbalimbali vya kutengenezea milipuko, pikipiki moja, baiskeli tatu, silaha mbalimbali za jadi ikiwemo mishale, pinde ,
visu na mapanga lakini hawakufanikiwa kukuta mtu.
Akizungumzia kuhusu watu hao kwamba ni kikundi cha wahalifu wa Alshabab au la, alisema mpaka sasa Polisi haijabaini kutokana na ukweli kwamba katika opereshi hiyo hawajafanikiwa kukamata mtu ambaye wanaweza kumfananisha na magaidi hao.
“Msako wetu unaendelea tunaomba wananchi watoe ushirikiano… kwa ukweli ni mapema sana kuthibitisha kwamba hao wahalifu ni wa kikundi cha Al-Shabab kama inavyodaiwa mitaani, kwa sababu mpaka sasa hatujatambua sura zao na kubaini ni watu wa aina gani,” alisema.
Alisema askari waliojeruhiwa, wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo na hali ya afya zao inaendelea vizuri.
Hata hivyo taarifa kutoka kwa chanzo cha kuaminika ndani ya Hospitali ya Bombo, imeeleza kwamba askari mmoja wa JWTZ amefariki dunia jana saa 8.30 mchana ingawa Chagonja amekataa kuthibitisha kifo hicho.
Licha ya kudai kwamba hali imerejea kuwa shwari, lakini mpaka sasa wako kazini na ulinzi umeimarishwa kuanzia katika eneo la Utofu lililoko umbali wa kilometa 5 kutoka mjini, ambapo askari wanaonekana kutaka kupata taarifa za kila mtu na magari yanayoendelea kutumia njia hiyo.
Mitaani hali ya ulinzi na usalama miongoni mwa wananchi katika halmashauri ya Jiji la Tanga, iliendelea kugubikwa na hofu kubwa na mashaka kutokana na mapigano yaliyokuwa yakisikika baina ya askari na kikundi cha wahalifu hao.
Mapigano hayo yalikuwa katika kitongoji cha Mikocheni kilichopo kata ya Kiomoni kwenye machimbo ya mawe ambayo yameambatana na eneo la Mapango ya Amboni.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa kata hiyo iliyoko umbali wa kilometa 10 kutoka katikati ya Jiji la Tanga, walianza kuona vurugu za magari ya askari wa kutuliza ghasia pamoja na JWTZ wakikatiza katika maeneo hayo huku ikisikika milio ya risasi na vishindo vikubwa.
Agata Juma, mkazi wa Kiomoni Majimoto, alisema vurugu hizo zilisababisha wapate hofu na kukumbuka tukio la hivi karibuni la mlipuko wa bomu la kurushwa kwa mkono, uliotokea wiki tatu zilizopita kwenye eneo hilo.
“Yani hatuelewi kinachoendelea, maana askari hawazungumzi kitu na wananchi bali tunasikia sauti za ving’ora pamoja na mishindo ya vitu kama mizinga mikubwa ikilia … mambo hayo yanafanyika huko jirani na mampango ya Amboni,” alidai.
Naye Jumaane Amboni, alidai usiku kucha hawakupata usingizi kutokana na hofu, hasa baada ya kupata taarifa ambazo hata hivyo hazijathibitishwa na Polisi, kwamba eneo hilo limevamiwa na kikundi cha Waislamu wenye itikadi kali wa Al-shabab.
“Usiku wa kuamkia leo mambo yalikuwa magumu sana mana tumesikia risasi zikirindima na vishindo kama vya mizinga vikilia mara kadhaa pasipo kuelewa cha kufanya…. tumeamua kukaa ndani na kujifungua.
“Tunachofanya hapa ni kujaribu kukusanya mahitaji ya muhimu kama chakula na vitu vingine, kwa sababu hatuelewi hayo mapigano yataisha lini hasa ikizingatiwa kwamba eneo walilojificha ni ndani ya sehemu ya mapango ya mawe ambayo hayatumiki kabisa,” alisema.
Hata hivyo baadhi ya wakazi katika maeneo ya katikati ya Jiji la Tanga, ingawa shughuli zinaendelea kama kawaida lakini wamekuwa katika hali ya wasiwasi.