Wednesday, February 4, 2015

Maskini Wajawazito Wajifungulia Sakafuni Kwenye Jengo la Wazi Huku Wengine Wakishuhudia

WAJAWAZITO katika Kijiji cha Msisi wilayani Bahi, mkoani Dodoma wanajifungulia sakafuni kwenye jengo la wazi, hali inayosababisha kukosa faragha.



Kutokana na kadhia hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa ameahidi kutoa Sh 500,000 kwa ajili ya kuchangia ujenzi za chumba cha kujifungulia akinamama hao.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Bahi, ambapo Diwani wa viti maalumu Kata ya Msisi, Dominica Nyau aliomba juhudi za makusudi zichukuliwe ili ujenzi wa wodi ya kujifungulia akinamama wajawazito ukamilike kutokana na wanawake hao kujifungulia sakafuni.

Alisema mwanamke anapojifungulia sakafuni hata usalama wa mtoto unakuwa ni mdogo kulingana na mazingira yake.

Alisema wanawake wanaofika kwa ajili ya kujifungua kwenye zahanati hiyo, wamekuwa wakijifungulia mahali ambapo hapana usiri kutokana kuuwepo na chumba ambacho hakimsitiri mwanamke kwa ajili ya shughuli hiyo.

Kwa mujibu wa diwani wa kata hiyo, Novemba Mosi, mwaka 2012, jengo la wodi ya kujifungulia katika zahanati ya kijiji hicho liliezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali, na kufanya akinamama kukosa mahali pa kujifungulia kutokana na ukarabati wake kuchukua muda mrefu.

Alisema juhudi mbalimbali zilifanyika ikiwamo kufikisha taarifa kwenye Baraza la Madiwani kupitia kamati za kudumu za afya, elimu na maji, ili halmashauri ifanye tathimini ambapo halmashauri iliomba Tamisemi kama maombi maalumu ili jengo hilo lifanyiwe ukarabati lakini ombi lao halikukubaliwa.

Licha ya kuomba juhudi kuchukuliwa kukamilisha ujenzi huo Mkwasa aliahidi kutoa Sh 500,000 na mifuko kadhaa ya saruji, ili kuhakikisa ujenzi huo wa wodi ya kinamama kujifungulia unakamilika.

Alisema akiwa kama mwanamke ameguswa na tatizo hilo kwani kujifungulia sakafuni wakati wa uchungu ni adhabu kubwa kwa akinamama