Mstaafu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege aliyekuwa akiishi Mbezi Makonde jijini Dar es Salaam, ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na mwili wake kushindiliwa kwenye friji (deep frizer) sebuleni kwake.
Joseph Minja (66) mmiliki wa baa ya Kunonze iliyoko Mbezi Makonde jijini, aliuawa baada ya watu wasiofahamika kumvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, ‘kumchinja’na kumwingiza kwenye friji licha ya miguu kubakia ikining’inia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kueleza kuwa Minja alikuwa akiishi na kijana ambaye jina lake halikufahamika.
Kwa mujibu wa Wambura, hakuna anayeshikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi unaendelea.
Habari zilizopatikana kutoka nyumbani kwa Minja zilisema kuwa, msaidizi wake pamoja na mtoto wa kiume ambaye wanaishi pamoja hawajulikani walipo.
Akizungumza na Paparazi Jumamosi, mmoja wa majirani waliokuwa kwenye msiba huo jana (jina linahifadhiwa), alisema Minja alikuwa mtumishi mstaafu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege . Alieleza kuwa mwili wake ulibainika siku ya pili baada ya tukio hilo.
Alisema baada ya watu hao wasiofahamika kumuua mzee huyo, Jumanne katika hali isiyo ya kawaida, mmoja wa majirani alipokea simu kutoka kwa mfanyakazi wa baa ya Kunonze iliyopo karibu na nyumba ya Minja akimpa ujumbe’ kuwa, “jana usiku walivamiwa na majambazi nyumbani lakini alifanikiwa kutoroka baada ya kukatwa panga la mkono.”
Alisema kijana huyo alimweleza jirani huyo kuwa, amepigiwa simu na mfanyakazi wa kazi wa mzee huyo.
“Kijana huyu wa baa alimweleza jirani huyo kuwa, mwenzake amemuomba ampigie simu ili aende nyumbani kwa Minja kuangalia hali ya mzee inaendeleaje baada ya tukio hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, alikwenda kwa Minja na kukuta mazingira yasiyo ya kawaida pamoja taa zikiwa zimezimwa akaona asichukue hatua kabla ya kuwaarifu majirani.
Baada ya kufika hapo, walichungulia dirishani na kuuona mguu wa mtu ukining’inia kwenye friji.
“Tuliwataarifu polisi na walipofika walikuta mwili wa Minja kwenye friji uliokuwa umeganda,” alisema.
Jirani mwingine (jina tunalo) alilieleza gazeti hili kuwa pembeni ya mlango wa kuingilia ndani kulikuwa na bomba la sindano lililotumika.
“Yaelekea watu hawa baada ya kumuua mzee Minja walikuwa wanajaribu kila njia ya kuuficha mwili wake, wamechimba hapa kwenye karo lakini bahati nzuri hii imesakafiwa kwa hiyo nahisi walivyoona zoezi ni gumu wakaamua kuuweka mwili wake kwenye friji,” alisema.
Jirani mwingine alisema kuwa, ndani ya nyumba katika meza ya chakula kulikutwa vyakula ambavyo ni wali, mbogamboga na kuku.
“Watu hawa yaelekea baada ya kula ndipo walipofanya mauaji haya ya kutisha na ya aina yake, wamemuondolea uhai mzee wetu kwa kifo cha kinyama na kikatili,” alisema na kuongeza:
“Vijana hawa waliokuwa wanakaa na kufanya kazi kwake, wanatakiwa kutafutwa wanaweza kuhusika kwa namna moja ama nyingine, kwa nini wamekimbia wote, sio wa baa wala wa nyumbani, hapa kuna kitu,” alisema.