Tuesday, February 10, 2015

WASAKA URAIS VIJANA: UTAFITI WAMNG'ARISHA MWIGULU NCHEMBA AKIFUATIWA NA ZITTO KABWE


Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Elimu (TEDRO),
limesema katika utafiti walioufanya kuhusu
ushiriki wa vijana katika siasa na matarajio
kuelekea uchaguzi mkuu 2015, umeonesha
kwamba endapo mgombea urais kijana
atapendekezwa atakubalika kwa asilimia 82.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa shirika hilo, Jacob Kateri
alisema katika wananchi hao waliohojiwa pia
asilimia 11 walisema vijana hawatakubalika na
asilimia saba walisema hawajui.
Alisema utafiti huo umeandaliwa na kufanyika
Tanzania Bara na maeneo yaliyohusishwa ni
kanda za kijiografia ili kuwezesha uhusishwaji
mpana wa Watanzania na katika kila wilaya
wamehojiwa wananchi wa vijiji vitatu kwa
kuzingatia siasa za eneo husika.
Aidha alisema utafiti huo umeonesha sababu
mbalimbali zinazoweza kuwa kichocheo cha
vijana kuingia katika siasa ambapo zilizochukua
uzito ni uzalendo kwa asilimia 67 ambapo
wananchi walisema vijana wengi wameingia katika
siasa kwa sababu ya uzalendo.
“Sababu nyingine ni kimbilio baada ya kukosa
ajira kwa asilimia 57, uwezo mdogo wa
watangulizi wao katika nafasi husika kwa asilimia
60, mafanikio ya wanasiasa vijana walio mahiri
asilimia 72, vyama vya siasa kuwapa nafasi vijana
katika vyama vyao kwa asilimia 59 na kukubalika
kwa vijana kwa asilimia 63,” alisema.
Aidha alisema wanasiasa vijana waliopendekezwa
kupitia chama tawala aliyeoonekana kuongoza
kwa kukubalika ni Mwigulu Nchemba kwa asilimia
38, Dk Emmanuel Nchimbi kwa asilimia 26,
January Makamba kwa asilimia 24, William
Ngeleja kwa asilimia 11 na Lazaro Nyalandu kwa
asilimia 10
Wengine ni Hamisi Kigwangala kwa asilimia saba,
Deo Filikunjombe kwa asilimia tano, Esther Bulaya
kwa asilimia 2 na waliosema hakuna anayefaa
walikuwa asilimia 9 na asilimia 13 walipendekeza
wengine wasio vijana.
Utafiti huo pia unaonesha kwamba kijana
anayepewa nafasi kubwa endapo atasimamishwa
kupitia upinzani anayeongoza ni Zitto Kabwe kwa
asilimia 18, James Mbatia kwa asilimia 16, Tundu
Lissu kwa asilimia 14, Halima Mdee kwa asilimia
nne na David Kafulila kwa asilimia sita.
Wengine ni Julius Mtatiro kwa asilimia nne, John
Mnyika kwa asilimia saba, Joshua Nassari kwa
asilimia mbili, Moses Machali kwa asilimia nne na
asilimia 11 ya wananchi walisema hawajui na
asilimia 16 walisema hawaoni anayefaa.
Hata hivyo, utafiti huo ulionesha kwamba endapo
wakishindanishwa vijana wote bila kujali itikadi
zao anayeongoza kwa kukubalika ni Mwigulu
Nchemba kwa asilimia 27, Zitto Kabwe kwa
asilimia 19, January Makamba kwa asilimia 14,
James Mbatia kwa asilimia 11 na Emmanuel
Nchimbi kwa asilimia nane.
Wengine ni Lazaro Nyalandu kwa asilimia saba,
Tundu Lissu kwa asilimia tano, Hamis Kigwangala
kwa asilimia nne, wengine waliotajwa wasio vijana
ni asilimia nne na wasiofaa walikuwa ni asilimia
mbili.
Mapema Mkurugenzi wa Mafunzo wa Utafiti wa
TEDRO, Jackson Coy alisema utafiti huo
wameufanya bila shinikizo kutoka kwa mtu yeyote
na waliufanya kuhusu siasa kutokana na kwamba
mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu.
Alisema lengo la utafiti huo limechambua ushiriki
wa vijana katika siasa kama wagombea, mchango
wa wanasiasa vijana katika kufuatia misingi ya
utawala bora na uwajibikaji, utekelezaji wa ahadi
za wagombea kwa wapiga kura na matarajio ya
wananchi kwa vijana katika kuelekea uchaguzi
mkuu.
“Utafiti tunaoendesha ni mwendelezo wa
uchambuzi wa changamoto za elimu, ndani ya
dira ya TEDRO na programu ya mchango wa
elimu katika kufungua fursa za ajira, siasa ikiwa ni
mojawapo ya fursa zenye kimbilio la vijana,”
alisema.
Hadi sasa TEDRO inaendesha utafiti wa Mitandao
ya Kijamii inavyoathiri wanafunzi wa sekondari na
kutazama njia rafiki katika kutumia mitandao hiyo
kama njia ya kujifunzia na kuendeleza sekta
nzima ya elimu.
Utafiti huu uliotarajiwa kuhusisha wilaya 24
Tanzania Bara, umeendeshwa katika wilaya 18,
kila wilaya ikiwa imewakilishwa na wahojiwa 45
waliochaguliwa 15 kutoka kila kijiji; hivyo utafiti
huu kuhusisha vijiji 54 kwa ujumla.
Wilaya ambapo utafiti umefanyika ni Njombe Mjini,
Ludewa, Mbeya Mjini, Kilwa, Lindi Mjini, Mtwara
Mjini, Morogoro Mjini, Kisarawe, Kinondoni, Tanga
Mjini, Vunjo, Arumeru, Singida, Kasulu, Kigoma
Mjini, Bukoba Vijijini, Biharamulo na Mwanza
Mjini (Nyamagana).
Katika utafiti huu uliohusisha watu 910, taarifa
binafsi za wahojiwa zilizokusanywa ni pamoja na
zile zinazohusu umri wa wahojiwa, jinsia, hali ya
ndoa, kazi, kiwango cha elimu na vyama vya
siasa vinavyoongoza majimbo sehemu uchaguzi
ulipofanyika.
Lakini wakati matokeo hayo ya utafiti yakianikwa,
kwa upande wa CCM, Rais Jakaya Kikwete hivi
karibuni akiwa mjini Songea, Ruvuma alikokuwa
mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 38 ya
chama hicho, alisema chama chake bado hakina
mgombea mpaka sasa.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania
kuwashawishi wanaoonekana kuwa na uwezo wa
kuongoza huku wakiwa hawana 'madoa’ waweze
kujitosa katika uchaguzi mkuu wa baadaye