Friday, April 3, 2015

GWAJIMA SASA ATIKISA NCHI, BAADA YA KUMTUKANA KADINALI PENGO!

KIONGOZI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima sasa anaitingisha nchi baada ya sakata lake lililotokana na kauli yake ya kejeli dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Policarb Kardinali Pengo kuwa gumzo karibu kila sehemu hapa nchini. 
Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, redio, magazeti na televisheni karibu zote sasa zinapambwa na habari za kuitwa kuhojiwa, kuzimia, kulazwa hospitalini na hatimaye kuachiwa na Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam mara tu baada ya kuwa ametoa maneno ya kashfa na kejeli kwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Gwajima alitoa kauli hiyo ya kashfa baada ya Askofu Pengo kupishana kauli na msimamo wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) ambao waliwataka waumini wao kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Kupiga Kura na baadaye kupiga kura ya hapana kuikataa Katiba Inayopendekezwa.
Pengo alitaka waumini kuachiwa wenyewe kuamua cha kufanya baada ya kuisoma katiba hiyo.
Kufuatia kauli hiyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilimtaka mchungaji huyo kujisalimisha ili ahojiwe juu ya matamshi yake hayo, kitu ambacho mtumishi huyo wa Mungu alikiri, lakini katikati ya mahojiano, ilidaiwa kuwa alipoteza fahamu na kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Polisi ya Baracks Kurasini kisha kuhamishiwa TMJ ambako alitibiwa kwa siku kadhaa na kuruhusiwa.

Wakati Askofu Pengo akisema hamjui mchungaji huyo mwenye wafuasi wengi na kutangaza kumsamehe, baadhi ya watu wamehusisha sakata hilo na mambo ya siasa, hasa kipindi hiki ambacho taifa liko njia panda kuhusu kupitishwa au kutopitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa, ambayo kura ya maoni imetajwa kupigwa Aprili 30, mwaka huu kote nchini.Gwajima jana alitarajiwa kufika Kituo cha Polisi Oysterbay kwa ajili ya mambo ya kisheria zaidi.