MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), wamesema hawajapata taarifa rasmi juu ya mgomo wa wamiliki wa mabasi ya mikoani.
Akizungumza na MPEKUZI kwa njia ya simu jana, Ofisa Habari wa Sumatra, Daud Mziray, alisema hakuna taarifa yoyote iliyowafikia ofisini kwao ya wanachama wa Taboa kugoma.
“Mimi niko mkutanoni Morogoro, mkutano wenyewe unahusiana na mambo ya ajali, hatujapata taarifa rasmi ya wanachama wa taboa kugoma,”alisema Mziray.
MPEKUZI ilimtafuta Katibu wa Taboa, Enea Mrutu, ili kuzungumzia suala hilo ambapo alisema kuwa tayari wameshapeleka barua yao Sumatara leo (jana) saa moja asubuhi na tamko lao ni lilelile waliloadhimia katika mkutano wao.
“Sumatra tumekwisha wapelekea barua toka saa moja asubuhi kama wanasema hawana tarifa wanadanganya kwasababu hata jana katika kikao chetu mwakilishi wao alikuwepo.
“Ingawaje kuna taarifa nimeipata kuwa Serikali inataka ifanye mazungumzo na sisi, tutakaa nao kama wataridhia kuacha nauli kama ilivyokuwa hatuna tatizo lakini wasipofikia muafaka na kutoa majibu ya kueleweka msimamo wetu utakuwa ni uleule,” alisema Mrutu.
Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani juzi katika mkutano wao walijadiliana juu ya kushuka kwa nauli na kuafikiana kutoshusha jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni kuitunishia misuli mamlaka hiyo.
Walisema endapo Sumatra hawatatoa majibu mapema kuanzia Aprili 29 mwaka huu (leo) hawatokata tiketi kwa wasafiri na badala yake wataendelea na mgomo huo kwa siku saba.
Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu, alisema SUMATRA ilikurupuka kushusha nauli bila kufanya mchanganuo na kuda.
Wamiliki hao waliafikiana kuwa yeyote atakayetoa gari lake kufanya biashara kabla hawajapata muafaka kutoka SUMATRA watamchukulia hatua za kisheria.
Aidha waliitaka serikali kurudisha viwango vya nauli za mabasi ya mikoani kwenye hali yake ya kawaida iliyokuwepo miezi michache iliyopita kwa sababu bei ya mafuta imerudi juu, baada ya kushuka kwa kisingizio cha bei ya mafuta kushuka.