WATOTO 140 wenye umri kati ya miaka 10 na 21 wamekamatwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wakilelewa katika misikiti mitatu tofauti. Taarifa zilizopatikana wilayani hapa zinasema watoto hao wamekuwa wakifundishwa mafunzo ya dini ya kiislam kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watoto hao waligundulika baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai kupata taarifa na kuwafuatilia kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kati ya Machi 25 na 27 mwaka huu.
Taarifa hizo zimeyataja maeneo waliyokutwa watoto hao kuwa ni Misikiti ya Masjid Bilal, Masjid Othiman na Msikiti wa Kwa Kiriwe.Taarifa hizo zimesema katika Msikiti wa Masjid Bilal uliopo Mtaa wa Kibaoni wilayani hapa, walikutwa watoto wa kiume 70 wanaotoka katika mikoa mbalimbali nchini.
Watoto wengine 50 wa kiume walikutwa katika Msikiti wa Masjid Othiman uliopo Mtaa wa Uzunguni ambao nao inasemekana wamekusanywa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa hizo zinasema watoto wengine 27 walikutwa katika Msikiti wa Kwa Kiriwe ambako pia walikuwa wakifundishwa mafunzo ya dini ya kiislam na walimu Watanzania. Mkuu wa Wilaya ya Hai, Anthoy Mtaka, alikiri kuwapo watoto hao wilayani kwake.
“Tukio hilo lipo na wanaohusika ni watu wanaotumia mwamvuli wa dini fulani kufanya mambo yasiyofaa katika jamii. “Kwa hiyo naziomba mamlaka husika likiwamo Baraza Kuu la Waisalam Tanzania (BAKWATA) kutambua miskiti na shughuli zinazoendelea katika nyumba hizo za ibada.
“Hili lazima walifanyie kazi kwa sababu hao vijana inasemekana wanafundishwa mazoezi makali ya kareti na judo katika nyumba hizo za ibada,” alisema Mtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alisema atazungumzia tukio hilo leo. Kupatikana kwa watoto hao ni mwendelezo wa matukio ya watoto wanaolelewa kinyume cha sheria mkoani Kilimanjaro baada ya matukio mawili ya aina hiyo kuripotiwa hivi karibuni. La kwanza lilihusisha watoto 18 na la pili lilihusisha watoto 11 waliokutwa katika maeneo ya Lyamungo wilayani Hai.
Chanzo: Mtanzania