Thursday, May 28, 2015

MAKUBWA:MBUNGE WA CHADEMA ATAKA BANGI IHALALISHWE KWA MATUMIZI YA TIBA NA CHAKULA

MBUNGE wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema),ameitaka Serikali kuufanyia utafiti mmea wa bangi ili kubaini iwapo unaweza kutumika kama dawa ya kutibu magonjwa ya binadamu.
 
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana Mtinda alisema iko mikoa ambayo bangi huota yenyewe kama vile Njombe, Iringa na Mara na kwamba wakazi ya mikoa hiyo huitumia kama chakula.
 
“Sasa ni utafiti gani ambao Serikali imeufanya kubaini iwapo mmea wa bangi unaweza kutumika kama dawa?” alihoji.

Aidha, aliitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi ambao wanaamini kwamba matumizi ya bangi yanaimarisha afya na kuongeza nguvu za kufanya kazi.
 
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alisema hakuna utafiti wowote utakaofanyika kwa mmea wa bangi kwa kuwa ni haramu na ni kinyume cha sheria.

“Serikali inasisitiza bangi ni haramu na matumizi yake ni kinyume na sheria hata kama bangi hiyo itakuwa imeota yenyewe, madhara ya bangi kwa nchi ni makubwa,” alisema.
 
Alisema pia hakuna utafiti ulioonyesha kwamba bangi inaongeza nguvu za aina yoyote ile.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema), Nkamia alisema Washington DC ni jimbo la tatu kupitisha matumizi ya bangi kama dawa kwa wagonjwa wenye maumivu sugu pamoja na kuliwaza watu walioumia katika ajali.
 
“Sheria hiyo ilianzia Jimbo la Alaska na Colorado ambao walishapitisha sheria hizo kwa matumizi ya kipimo kisichozidi gramu 56 kwa mtumiaji mwenye umri kati ya miaka 21 na kuendelea.

“Halikadhalika mtumiaji hapaswi kuvuta mbele ya kadamnasi, kuuza wala kusafirisha na akifanya hivyo ni kosa la jinai na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake,” alisema.
 
Alisema msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kwamba inafuata sheria ambayo inaeleza kwa kina kuwa mtu yoyote atakayejihusisha na kutumia, kuhamasisha matumizi,kuuza, kusafirisha, kuhifadhi na kujihusisha kwa namna yoyote ile na bangi ni kosa la jinai.

Alisema adhabu kwa makosa hayo hufikia hadi kifungo cha maisha. Katika swali lake Nyerere alitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu kuhalalishwa kwa matumizi ya bangi kwa Serikali ya Washing DC Marekani.